Russia na Ufaransa kuendelea kufungamana na JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/world-i44534-russia_na_ufaransa_kuendelea_kufungamana_na_jcpoa
Siku chache baada ya Rais Donald Trump kutangaza kuiondoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya Iran yanayofahamika kama JCPOA, kwa mara nyingine tena marais wa Russia na Ufaransa wamesisitizia umuhimu wa pande zilizosalia kuendelea kufungamana na mapatano hayo ya kimataifa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 15, 2018 22:11 UTC
  • Russia na Ufaransa kuendelea kufungamana na JCPOA

Siku chache baada ya Rais Donald Trump kutangaza kuiondoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya Iran yanayofahamika kama JCPOA, kwa mara nyingine tena marais wa Russia na Ufaransa wamesisitizia umuhimu wa pande zilizosalia kuendelea kufungamana na mapatano hayo ya kimataifa.

Katika mazungumo yao ya simu jana Jumanne, Rais Vladimir Putin wa Russia na mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron wamesema mazungumzo yao yamejikita zaidi kuhusu hatua ya upande mmoja ya Washington ya kujiondoa kwenye makubaliano hayo yaliyofikiwa kati ya Iran na Kundi la 5+1 mjini Vienna Julai mwaka 2015 na kuanza kutekelezwa Januari 2016.

Rais Putin amemtaarifu Rais Macron kuhusu mkutano na mazungumzo yake ya juzi Jumatatu Mei 14 mjini Sochi, na Yukiya Amano, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA.

Kadhalika marais hao wa Ufaransa na Russia wamebadilishana mawazo kuhusu njia za kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Syria.

Trump baada ya kuiondoa Marekani kwenye makubaliano ya JCPOA

Siku chache zilizopita, Federica Mogherini Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya alisisitiza kuwa makubaliano ya JCPOA yalikuwa yenye mafanikio na kwamba Umoja huo una azma thabiti ya kuyalinda.

Alisisitiza kuwa, "Hakuna nchi inayoweza kuyafuta makubaoiano hayo kwa upande mmoja kwa sababu makubaliano hayo si makubaliano ya pande mbili pekee bali ni urithi wa kimataifa."

Hatua hiyo ya upande mmoja ya Trump imeendelea kupingwa na kulalamikiwa vikali na pande tofauti duniani.