Kimbunga chaua watu 47 nchini India, joto laongezeka
Watu wasiopungua 47 wamepoteza maisha kutokana na kimbunga kikali kilichoshuhudiwa kaskazini mwa India.
Idara ya Kupambana na Majanga nchini humo imesema kimbunga hicho kimesababisha maafa hayo katika majimbo ya Uttar Pradesh, Bihar na Jharkhand.
Yoginder Singh, afisa wa idara hiyo ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, kimbunga hicho kikali kiliandamana na radi na kusababisha maafa hayo haswa katika eneo la Bihar. Habari zaidi zinasema kuwa, watu 11 wameaga dunia baada ya kupigwa na radi.
India inashuhudia majanga hayo ya kimaumbile wakati huu ambapo nchi hiyo inashuhudia joto kali, huku kiwango cha nyuzijoto kikiripotiwa kupindukia 48.6.
Mapema mwezi huu, wimbi jingine la vimbunga, radi na mafuriko yaliyoikumba India lilisababisha vifo vya watu wasiopungua 143 katika maeneo ya Uttar Pradesh, Rajasthan, Uttarakhand na Punjab.