Hatua mpya za Ulaya kulinda makubaliano ya JCPOA
Sambamba na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutangaza hatua ya kuimarisha shughuli zake za nyuklia katika fremu ya mapatano ya nyuklia na nchi sita kubwa za dunia mashuhuri kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA), nchi za Ulaya zimeongeza mashauriano na juhudi za kuyalinda yasije yakasambaratika.
Miongoni mwa mashauriano na juhudi hizo za kujaribu kulinda mapatano hayo ni barua ya pamoja iliyoandikwa na mawaziri wa mambo ya nje na fedha wa nchi za Ujerumani, Uingereza na Ufaransa tarehe 4 mwezi huu, na kutiwa saini na Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Ulaya, kwa wenzao wa Marekani wakibainisha wasiwasi wao kuhusiana na hatari ya uwezekano wa Iran kujiondoa katika mapatana hayo, na kuitaka serikali ya Washington isiyawekee vikwazo mashirika ya kigeni yanayofanya biashara na Iran. Mawaziri hao wamewaambia viongozi wa Marekani kwamba uwezekano wa Iran kujitoa kwenye mapatano hayo kunaweza kuvuruga zaidi usalama wa Mashariki ya Kati. Msimamo huo umechukuliwa na nchi za Ulaya katika hali ambayo hapo siku ya Jumatatu Shirika la Atomiki la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran liliuandikia barua Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia IAEA likiufahamisha kuwa serikali ya Tehran ina nia ya kuongeza kiwangio cha urani yake uliyorutubishwa katika fremu ya makubaliano ya JCPOA.
Akizungumza Jumatatu Atyatullah Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzo ya Kiilsmau alilitaka shirika hilo la nishati ya nyuklia kuanzisha mara moja utangulizi unaohitajika kwa ajili ya kurutubisha urani kwa kiwango cha SWU laki moja na 90 elfu kwa mujibu wa mapatano ya nyuklia ya JCPOA. Hatua hiyo ambayo inaoonyesha kuwa Iran iko tayari kujiondoa katika mapatano ya JCPOA iwapo maslahi yake hayatadhaminiwa, imewatia wasiwasi mkubwa viongozi wa Ulaya. Akizungumzia suala hilo Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amesema kuwa anafahamu kwamba hatua hiyo ya Iran imetekelezwa katika misingi ya sheria lakini akaongeza kuwa ana wasiwasi kwamba huenda ikaongeza mivutano. Wakati huohuo siku ya Jumatano, Kamisheni ya Umoja wa Ulaya ilisasisha (update) sheria ambazo zitaziwezesha nchi wanachama wa umoja huo kukabiliana na matokeo ya vikwazo vya Marekani dhidi ya masharika ya Ulaya yanayofanya biashara na Iran.
Sheria hizo zilizopitishwa mwaka 1996 kwa ajili ya kukabiliana na vikwazo vya Marekani dhidi ya Cuba, hazikuwahi kutekelezwa kivitendo. Hivyo zilihitaji kurekebishwa na kusasishwa ili ziweze kutekelezwa wakati wa dharura kuhusiana na Iran. Ikiwa hakuna mwanachama yeyote wa Umoja wa Ulaya atakayezipinga, basi zitaanza kutekelezwa mwezi Agosti mwaka huu sambamba na kuanza kutekelezwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran. Sheria hizo zinaziwezesha nchi za Ulaya kutozingatia sheria za nje za Marekani ambazo zinayakandamiza mashirika ya kigeni na kuyataka pia yadai fidia iwapo yatadhurika kutokana na sheria hizo za upande mmoja za Marekani. Kamisheni hiyo ya Ulaya pia imeitaka Benki ya Uwekezaji ya Ulaya kuwadhamini wawekezaji wa Ulaya wanaojishughulisha na miamala ya kibiashara na kiuchumi nchini Iran. Hivyo ni wazi kuwa juhudi mpya zinazofanywa na Ulaya zimelenga kulinda makubaliano ya JCPOA. Si nchi za Ulaya tu bali wanachama wote wa mapatano ya JCPOA wanapasa kuweka wazi kwa mara ya mwisho msimamo wao kuhusiana na hatua ya kibabe na ya upande mmoja ya Marekani kujiondoa katika mapatano hayo muhimu ya kimataifa.
Kuhusu hilo, tayari Angela Merkel, Kansela wa Ujerumani amesema kuwa tofauti zilizopo kati ya nchi za Ulaya na Marekani kuhusu makubaliano ya JCPOA ni kubwa. Mapatano hayo ambayo kimsingi yalifikiwa kwa ajili ya kutatua masuala ya nyuklia baina ya Iran na nchi za kundi la 5+1 tayari yamekuwa na matokeo ya kuridhisha. Kwa msingi huo ni wazi kuwa kuvunjika kwa mapatano hayo kutakuwa na madhara makubwa kwa nchi za Ulaya. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imethibitisha nia yake njema kwa kutekeleza ahadi zake zote kuhusiana na mapatano hayo na sasa ni wakati wa Ulaya kuonyesha kuwa imeazimia vilivyo kulinda maslahi yake ya kiuchumi na kiusalama kwa kutekeleza yale yote yaliyoafikiwa katika mapatano hayo.