Jun 12, 2018 08:17 UTC
  • Al Azhar yalaani wito wa kufutwa aya za Qur'ani

Sheikh Mkuu wa Al Azhar nchini Misri, Ahmad Tayyib amekosoa vikali wito uliotolewa na kundi la eti wasomi na wanasiasa wa Ufaransa wa kufutwa aya za Qur'ani tukufu.

Sheikh Ahmad al Tayyyib amesema kuwa kuyavunjia heshima matukufu ya kaumu nyingine ni miongoni mwa sababu za ugaidi na katika masuala yanayoshajiisha mapigano na umwagaji wa damu za watu wasio na hatia.

Akijibu wito uliotolewa na baadhi ya wasomi na wanasiasa wa Ufaransa waliotaka kufutwa baadhi ya aya za kitabu kitukufu cha Qur'ani, Sheikh wa al Azhar amesema: Katika Qur'ani hakuna aya zinazohimiza kuua Mayahudi na Wakristo na kwamba aya zinazohusiana na maudhui hiyo zinazungumzia umuhimu na wajibu wa kujihami na kukabiliana na uvamizi wa maadui.

Dakta al Tayyib amesisitiza kuwa, wito wa wanasiasa wa Ufaransa wa kufutwa aya na baadhi ya sura za Qur'ani ni sehemu ya mashambulizi yanayoendelea tangu karne 14 zilizopita kwa ajili ya kuchafua sura ya kitabu kitakatifu cha Qur'ani na kuwafanya watu wachukie kitabu hicho na mafundisho yake.

Matukufu ya Kiislamu yanahujumiwa nchini Ufaransa

Makala ya dharau na iliyo dhidi ya Uislamu ambayo ilichapishwa katika gazeti la Le Parisien mjini Paris tarehe 22 Aprili, ilisainiwa na rais wa zamani wa nchi hiyo, Nicolas Sarkozy, aliyekuwa waziri mkuu Manuel Valls na watu wengine 300.

Hatua kama hizi za waandishi wa Magharibi za kuhujumu Uislamu na kitabu kitakatifu cha Qur'ani zimekuwa zikishuhudiwa mara kwa mara katika nchi za Ulaya.

Miaka kadhaa iliyopita Salman Rushie wa Uingereza aliandika kitabu alichokipa jina la "Aya za Shetani" akihujumu matukufu ya Kiislamu kikiwemo kitabu kitakatifu cha Qur'ani. Vilevile gazeti la Charlie Hebdo na huko huko Ufaransa liliwahi kumvunjia heshima Mtume Muhammad (saw).

Tags