China yajibu mapigo ya Marekani katika vita vya kibiashara
Serikali ya China imetangaza kupandisha ushuru wa forodha kwa asilimia 25, kwa bidhaa 659 za Marekani zinazoingia nchini humo, ikiwa ni katika kujibu hatua ya kiuhasama ya Washington ya kutangaza ongezeko la ushuru kwa asilimia 25 kwa bidhaa za China zinazopelekwa nchini Marekani, lililotangazwa na Rais Donald Trump mapema jana Ijumaa.
Wizara ya Biashara ya China imesema ongezeko hilo la ushuru wa forodha linahusu bidhaa za kilimo zenye thamani ya dola bilioni 34, na bilioni 16 kwa bidhaa kama mafuta ghafi, gesi asilia na mkaa zinazoingia nchini humo kutoka Marekani.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, inashangaza kuona Marekani jinai inavyopuuza maslahi ya China na kuamua kuchukua hatua za upande mmoja zinazokiuka miongozo na kanuni za Shirika la Biashara Duniani WTO.
Hii si mara ya kwanza kwa Beijing na Washington kutunushiana misuli katika uga wa biashara.
Mwezi Machi mwaka huu, ikiwa ni jibu la serikali ya China kwa hatua ya Marekani ya kuzipandishia ushuru wa asilimia 500 bidhaa za vyuma na alumini zinazoingizwa nchini humo kutoka China, Beijing ilizipandishia bidhaa 106 za Marekani zinazoingia nchini humo ushuru wa forodha wa asilimia 25.
Hata kabla ya kuingia madarakani, Donald Trump amekuwa akiithumu China kuwa ni 'mwizi wa fursa za kazi nchini Marekani' na aliapa kuangalia upya sera za biashara za Marekani na haswa miamala ya kibiashara na nchi hiyo ya bara Asia.