Kufunguliwa kambi kubwa ya kijeshi ya Marekani nchini Korea Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/world-i46494-kufunguliwa_kambi_kubwa_ya_kijeshi_ya_marekani_nchini_korea_kusini
Licha ya Rais Donald Trump wa Marekani kutangaza azma ya kutaka kupunguza askari wa nchi hiyo katika eneo la Peninsula ya Korea, serikali ya Washington imefungua kambi kubwa zaidi ya kijeshi duniani karibu na Seoul, mji mkuu wa Korea Kusini.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 01, 2018 11:26 UTC
  • Kufunguliwa kambi kubwa ya kijeshi ya Marekani nchini Korea Kusini

Licha ya Rais Donald Trump wa Marekani kutangaza azma ya kutaka kupunguza askari wa nchi hiyo katika eneo la Peninsula ya Korea, serikali ya Washington imefungua kambi kubwa zaidi ya kijeshi duniani karibu na Seoul, mji mkuu wa Korea Kusini.

Ijumaa iliyopita Jenerali Vincent Keith Brooks, kamanda wa vikosi vya Marekani nchini Korea Kusini alitangaza katika sherehe za ufunguzi wa kambi hiyo kwamba, imepangwa kuwa karibu askari elfu 43 wa Marekani na familia zao wataishi katika kambi hiyo kufikia mwishoni mwa mwaka 2022. Ufunguzi wa kambi hiyo kubwa ya kijeshi umejiri katika hali ambayo, katika kikao cha tarehe 12 mwezi huu wa Juni na Kim Jong-un wa Korea Kaskazini nchini Singapore, Rais Donald Trump wa Marekani aliahidi kusimamisha maneva ya kijeshi kati ya nchi yake na Korea Kusini sambamba na kupunguza idadi ya askari wa nchi hiyo huko Korea.

Wakati Trump alipokutana na Kim Jong-un aliahidi kupunguza idadi ya askari wa Marekani huko Korea

Kambi hiyo ya kijeshi iko umbali wa kilometa 70, kusini mwa mji wa Seoul, katika eneo la Pyeongtaek. Aidha ufunguzi wa kambi hiyo kubwa ya kijeshi ya Marekani nchini Korea Kusini ambao umeenda kinyume na ahadi aliyoitoa Trump akiwa na Kiongozi wa Korea Kaskazini nchini Singapore, ni ishara ya kutoheshimu mikataba inayotiwa saini na ikulu ya Marekani (White House) na kadhalika ni mgongano wa maneno na matendo ya rais huyo wa Marekani kuhusiana na ahadi yake ya kupunguza mzozo ndani ya Peninsula ya Korea. Kwa mtazamo wa Pyongyang, uwepo wa kijeshi wa Marekani katika eneo la Korea ni uchochezi na tishio kwa usalama wa Korea Kaskazini na ni kwa ajili hiyo ndipo katika mwenendo wa mazungumzo na Marekani na pia Korea Kusini kwa ajili ya kupunguza mzozo, ikasisitiza kusimamishwa maneva ya pamoja ya nchi hizo mbili na pia kuhitimishwa uwepo wa kijeshi wa nchi hiyo ndani ya eneo hilo.

Ushirikiano wa Korea Kusini na Marekani licha ya raia wa Korea kupinga uhusiano huo

Kadhalika kusimamishwa maneva ya pamoja kati ya Marekani na Korea Kusini na baadhi ya nchi za eneo sambamba na ufunguzi wa kambi kubwa ya kijeshi ya Marekani nchini Korea Kusini, umebainisha kwamba katika mipango yake ya kistratijia ndani ya Rasi ya Korea, Washington haina nia ya kuacha kuwepo kijeshi katika eneo hilo. Siasa hizo za Marekani ambazo zinahesabiwa kuwa chanzo kikuu cha kushtadi mzozo katika eneo la Korea, zinatekelezwa katika hali ambayo ilitarajiwa kuwa White House baada ya duru ya kwanza ya mazungumzo kati ya Rais Donald Trump na Kim Jong-un nchini Singapore, ingekuwa ya kwanza kufanya juhudi za kupunguza mzozo wa eneo tajwa. Kwa upande mwingine ni kwamba kufunguliwa kambi hiyo kubwa ya kijeshi na Marekani, mbali na kwamba kunaweza kuikasirisha Korea Kaskazini kutokana na ukiukaji ahadi wa Marekani kuhusiana na suala la kupunguza uwepo wake wa kijeshi katika Rasi ya Korea, pia kunaweza kuathiri mazungumzo yajayo kati ya viongozi wa Pyongyang na Washington.

Licha ya Ppyongyang kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano na mahasimu wake, lakini bado mahasimu hao hawajaonyesha nia njema

Hii ni katika hali ambayo Korea Kusini kubebeshwa gharama kubwa ya uendeshaji wa kambi hiyo kutokana na Marekani kujitanua kijeshi katika eneo hilo, ni jambo ambalo linapingwa vikali na wananchi wa Korea Kusini. Hivi karibuni Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kusini ilitangaza kwamba, haitakubali kugharamia siasa za kujitanua Marekani katika eneo na kwamba itakubali tu kuchangia gharama zinazokubalika kuhusiana na suala hilo. Katika uwanja huo, mhariri mkuu wa gazeti la Japan Times ameandika: "Kwa kupeleka askari wake katika Peninsula ya Korea, Marekani haina lengo la kuilinda Korea Kusini wala Japan, bali ni kwa ajili ya kulinda maslahi yake ya kistratijia katika eneo la mashariki mwa Asia kama vile kudhibiti vyanzo vya maji vya nchi za eneo hilo, na kwa msingi huo Washington haipasi kuzibebesha nchi nyingine gharama zake za kijeshi." Kwa kuzingatia ahadi za Rais Moon Jae-in wa Korea Kusini kuhusiana na kuchukua stratijia za kupunguza mzozo na Korea Kaskazini sambamba na kuepusha visababishi vya mizozo katika eneo, hivyo wananchi wa Korea Kusini wanataraji kwamba viongozi wao watajiepusha na hatua zozote za Marekani ambazo zinavuruga mwenendo wa kuboresha uhusiano wa nchi yao na nchi jirani ya Korea Kaskazini.