China yawaonya raia wake dhidi ya kwenda Marekani, kisa usalama
https://parstoday.ir/sw/news/world-i46539-china_yawaonya_raia_wake_dhidi_ya_kwenda_marekani_kisa_usalama
China imetoa tahadhari mpya kwa raia wake waliosafiri au wanaotaka kusafiri kwenda Marekani ikisema kuwa hakuna usalama wa umma nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 03, 2018 11:03 UTC
  • China yawaonya raia wake dhidi ya kwenda Marekani, kisa usalama

China imetoa tahadhari mpya kwa raia wake waliosafiri au wanaotaka kusafiri kwenda Marekani ikisema kuwa hakuna usalama wa umma nchini humo.

Ubalozi wa Beijing mjini Washington umewataka watalii raia wa China kuwa macho kutokana na kudorora usalama wa umma nchini Marekani, haswa kuongezeka visa vya ufyatuaji risasi kiholela na watu kushambuliwa na kuporwa.

Ubalozi huo umewashauri Wachina kujiepusha na safari za Marekani isipokuwa za dharura, kutokana na nukta kadhaa, kama vile gharama za juu za matibabu, kupekuliwa kupita kiasi au hata kukamatwa na maafisa wa forodha, mawasiliano yao kudukuliwa na kukithiri majanga ya kimaumbile.

Taarifa ya ubalozi wa China mjini Washington imesema: Wasafiri wawe macho na makini katika mazingira yao na watu walio karibu nao hapa Marekani. Wajiepusha kwenda nje wakiwa peke yao nyakati za usiku, kwani kesi za ufyatuaji risasi ovyo na wizi wa mabavu zinaonekana mara kwa mara.

Vita vya kibiashara kati ya China na Marekani

Wizara ya Mambo ya Nje ya China inasisitiza kuwa, tahadhari hiyo haijatolewa katika misingi ya kisiasa, bali usalama wa raia wao.

Haya yanajiri katika hali ambayo, katika siku za hivi karibuni, Beijing na Washington zimeoneka kutunushiana misuli katika uga wa biashara. Mwezi uliopita wa Juni, serikali ya China ilitangaza kupandisha ushuru wa forodha kwa asilimia 25, kwa bidhaa 659 za Marekani zinazoingia nchini humo, ikiwa ni katika kujibu hatua ya kiuhasama ya Washington ya kutangaza ongezeko la ushuru kwa asilimia 25 kwa bidhaa za China zinazopelekwa nchini Marekani.