Kutuhumiwa ubalozi wa Marekani mjini Kabul, katika kueneza silaha haramu
Kamanda wa Usalama mjini Kabul, mji mkuu wa Afghanistan, ameutuhumu ubalozi wa Marekani nchini humo kwamba unahusika katika kueneza silaha zilizopigwa marufuku.
Mohammad Davood Ramin, amesema kuwa, wamiliki wa silaha haramu ambazo zilinaswa na polisi ya nchi hiyo mjini Kabul, walizipata kupitia ubalozi wa Marekani. Hivi karibuni maafisa usalama nchini Afghanistan walinasa makontena kadhaa yaliyokuwa na silaha za magendo katika maeneo tofauti ya mji wa Kabul, silaha ambazo zilikuwa zikipelekwa maeneo yasiyojulikana. Aidha viongozi wa shirika moja la kigeni kupitia ubalozi wa Marekani, wamenaswa na kukabidhiwa ofisi ya kamanda wa usalama wa mji huo, hata hivyo jina la shirika hilo la kigeni halikuwekwa wazi. Kabla ya hapo pia vyanzo vya habari nchini humo viliripoti kwamba makundi ya kigaidi yanajizatiti kwa silaha za kisasa yanazozipata kutoka kwa Marekani. Aidha kugunduliwa na kunaswa na polisi ya Afghanistan makontena yaliyokuwa na silaha haramu na ambazo ubalozi wa Marekani umetajwa kuhusika nazo, ni uthibitisho mwingine wa hatua haribifu za nchi hiyo ya Magharibi nchini humo.
Kabla ya hapo kulitolewa ripoti ambazo zilionyesha kwamba helikopta za Marekani zimekuwa zikiwabeba wanachama na viongozi wa kundi hatari la kigaidi la Daesh (ISIS) nchini humo. Katika uwanja huo, Zamir Kabulov, mjumbe maalumu wa Russia katika masuala ya Afghanistan sambamba na kuonyesha masikitiko yake juu ya mwenendo wa kubebwa na kuhamishiwa maeneo tofauti ya Afghanistan, wanachama wa kundi la Daesh na helikopta za kutiliwa shaka, alisema kuwa, wawakilishi wa bunge la nchi hiyo wanazitambua helikopta hizo kuwa ni za Marekani. Kadhalika Kabulov aliutaka Umoja wa Mataifa uanzishe uchunguzi kuhusiana na suala hilo. Hata hivyo hatua za uharibifu za Marekani nchini Afghanistan haziishii katika mwenendo huo, bali ni zenye wigo mpana na wenye kutia wasi wasi mkubwa. Kuhusiana na suala hilo, shirika la kiusalama la Marekani na utawala haramu wa Kizayuni la Blackwater na katika kipindi cha utawala wa Hamid Karzai, rais wa zamani wa nchi hiyo lilituhumiwa kuanzisha jela maalumu za mateso na kadhalika magendo ya silaha nchini Afghanistan. Shirika hilo kwa kisingizio cha kutoa huduma za kiusalama, lilitenda jinai mbalimbali yakiwemo mauaji yaliyoratibiwa dhidi ya raia wa Afghanistan na Iraq, na hatimaye likalazimika kufungasha virago kutoka nchi hizo baada ya kufichuliwa jinai zake na kufuatia mashinikizo ya ndani ya nchi hizo.
Shirika la Blackwater lilifikia hatua ya kutoa pendekezo la kutia shaka la kutaka kuchukua nafasi ya askari wa Marekani kwa kutuma maafisa wake wapatao 5500 nchini Afghanistan, suala ambalo lilikabiliwa na radiamali kali kutoka kwa viongozi wa nchi hiyo. Sin McFaith, mwandishi wa kitabu kinachozungumzia sakata la shirika hilo anasema: “Pendekezo la shirika la Blackwater lilikuwa hatari sana na la kijinga ambalo lilikuwa linaufanya mwenendo wa vita vya Afghanistani usiweze kutabirika.” Kwa ajili hiyo na kwa kuzingatia historia mbaya ya jeshi la Marekani na mashirika ya kiusalama ya nchi hiyo katika kuhatarisha usalama na uthabiti wa Afghanistan, kunaswa makontena yaliyosheheni silaha haramu na ambazo zinahusishwa na ubalozi wa Marekani mjini Kabul, kunadhihirisha uwepo wa siasa za uhasama za Washington dhidi ya raia wa nchi hiyo ya Asia ya Kati. Ukweli ni kwamba msaada wa silaha wa Marekani kwa makundi ya kigaidi nchini Afghanistan, ni miongoni mwa mambo yanayoweza kuendeleza vita vya ndani nchini humo na hivyo kuiandalia White House mazingira ya kufikia malengo yake machafu na ya muda mrefu ndani ya taifa hilo masikini.