Russia yaitaka jamii ya kimataifa kutegua mabomu ya ardhini nchini Syria
Russia imezitolea wito nchi mbalimbali ziisaidie Moscow kutegua mabomu ya ardhi katika maeneo yaliyokombolewa kutoka mikononi mwa magaidi huko Syria.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imetoa taarifa ikikaribisha kusainiwa hati ya ushirikiano kati ya serikali ya Syria na Shirika la Kutegua Mabomu la Umoja wa Mataifa na kusisitiza kuwa, msaada huo utasaidia kuandaliwa hali nzuri na salama kwa ajili ya kurejea nyumbani mamilioni ya wakimbizi wa Syria na kuijenga upya nchi hiyo.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imeutaja ushiriki wa Umoja wa Mataifa katika kutegua mabomu huko Syria kuwa ni kuendelezwa vyema jitihada za Russia katika uwanja huo na kukumbusha kuwa, hadi kufikia sasa Russia imeshategua mabomu katika maeneo ya Tadmir, Halab na Deir-Zor huko Syria.
Itakumbukwa kuwa baada ya kuyavamia na kuyakalia maeneo ya Tadmir, Halab Deir-Zor na mengineyo ya Syria, magaidi walizigeuza nyumba za raia, maeneo ya umma, magari, baiskeli na hata wanasesere wa kuchezea watoto kama vifaa vya kutegea mabomu na mada za milipuko.