Uswizi yaishtaki Marekani WTO kutokana na ushuru wa forodha
Uswizi imewasilisha lalamiko rasmi katika Shirika la Biashara Duniani WTO dhidi ya hatua ya Marekani ya kutoza kiwango kikubwa kupita kiasi cha ushuru wa forodha kwa bidhaa za chuma na bati kutoka barani Ulaya.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Uchumi ya Uswizi inasema ushuru mpya wa forodha unaotozwa na Marekani si wa haki. Uswizi, ambayo ni nchi ya nane mwanachama wa WTO kuwasilisha malalamiko dhidi ya Marekani, inasema mwaka jana iliuza bidhaa za chuma na bati zenye thamani ya dola milioni 80.7 nchini Marekani.
Taarifa hiyo imesema Marekani imekataa kujibu ombi la Uswizi la kuondolewa ushuru huo na hivyo shtaka hilo limewasilishwa kwa WTO kulinda maslahi ya Uswizi. Aidha Uswizi imetahadharisha kuwa itachukua hatua za kulipiza kisasi dhidi ya bidhaa za Marekani zinazoingizwa nchini humo. Marekani pia imeongeza ushuru unaotozwa magari yanayoingizwa nchini kutoka bara Ulaya na bidhaa nyiginezo kutoka China na maeneo mengine duniani.

Katika hatua inayoashiria kuanza vita vya kibiashara, China nayo hivi karibuni imetangaza ushuru wenye thamani ya dola bilioni 50 kwa bidhaa zinazotoka Marekani, ikilipiza kisasi cha ongezeko jipya la ushuru lililotangazwa na Marekani.
Zaidi ya nchi 40 wanachama wa WTO, zikiwemo nchi 28 za Umoja wa Ulaya zimeonya kuwa sera hizo za Marekani kuhusu ushuru wa forodha zitavuruga soko la dunia na ni tishio kwa mfumo wa WTO.