Dogu Perinçek: Uturuki ni lazima ishirikiane na Iran
https://parstoday.ir/sw/news/world-i46775-dogu_perinçek_uturuki_ni_lazima_ishirikiane_na_iran
Mkuu wa chama cha Patriotic nchini Uturuki, amesisitiza juu ya ulazima wa nchi hiyo kushirikiana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hata baada ya Tehran kuwekewa vikwazo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 14, 2018 09:29 UTC
  • Dogu Perinçek: Uturuki ni lazima ishirikiane na Iran

Mkuu wa chama cha Patriotic nchini Uturuki, amesisitiza juu ya ulazima wa nchi hiyo kushirikiana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hata baada ya Tehran kuwekewa vikwazo.

Dogu Perinçek amesema Ankara ina wadhifa wa kusimama imara mkabala wa mashinikizo ya Marekani na utawala wa Kizayuni kuhusiana na nchi rafiki na jirani zake hususan Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ameongeza kwa kusema, katika njama za kufikia malengo yao ndani ya eneo la Mashariki ya Kati, Marekani na utawala haramu wa Israel zinakusudia kuzidhoofisha serikali za nchi za eneo hili, kupitia jaribio lililofeli la mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika tarehe 15 Julai mwaka 2016 nchini Uturuki ambayo yalikuwa na lengo la kuibua fitina nchini humo kwa kuifanya Uturuki kuwa nchi isiyokuwa na uthabiti.

Dogu Perinçek, Mkuu wa chama cha Patriotic nchini Uturuki

Mkuu wa chama cha Patriotic nchini Uturuki, amesema kuwa mpatano ya nyuklia ya Iran yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji, JCPOA yalikuwa mafanikio muhimu ya kihistoria na kimataifa na kwamba kitendo cha Marekani cha kujiondoa katika mapatano hayo, ulikuwa ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa. Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kuiondoa nchi yake katika mapatano ya nyuklia ya Iran tarehe 8 Mei mwaka huu kupitia tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambapo baada ya kutangaza hatua hiyo aliahidi kurejesha vikwazo dhidi ya Tehran. Hatua hiyo ya upande mmoja ya Marekani ilikabiliwa na ukosoaji mkali ndani na nje ya Marekani zikiwemo pia nchi washirika wa Washington. Wakati huo huo, Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki ametangaza kuanza shughuli za kibiashara kwa kutumia sarafu za taifa hilo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Russia na China. Erdoğan amesisitiza kuwa, uamuzi huo ni wa dhati na una lengo la kukabiliana na athari mbaya zinazotokana na fedha za kigeni zilizozoeleka katika mfumo wa biashara kimataifa.