Japan yasisitiza kuendelea kununua mafuta ya Iran
Waziri wa Uchumi, Biashara na Viwanda wa Japan amesisitiza kufanyika juhudi za kuendelea kuagiza mafuta kutoka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Hiroshige Seko ameyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari mjini Tokyo, mji mkuu wa Japan na kuongeza kuwa, serikali ya nchi hiyo inaendelea kuishinikiza Marekani kwa lengo la kuendelea kuagiza mafuta kutoka Iran. Matamshi ya Hiroshige Seko yametolewa katika hali ambayo, viongozi wa kituo cha kusafishia mafuta cha Japan wameitaka serikali ya nchi hiyo kufuatilia kuondelewa katika uga wa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran, kwa kuwa kituo hicho kinataka kuendelea kuagiza kiwango cha kawaida cha mafuta kutoka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran badala ya kupunguzwa kiwango hicho.
Baada ya serikali ya Marekani kujiondoa katika mapanato ya nyuklia ya JCPOA hapo mwezi Mei mwaka huu, imedai kutaka kufanya uuzaji nje mafuta ya Iran kufikia sifuri, kwa kuzitaka nchi za dunia kuacha kununua nishati hiyo muhimu kutoka Iran, kuanzia tarehe nne Novemba mwaka huu suala ambalo limeendelea kupingwa na nchi nyingi. Katika uwanja huo hivi karibuni pia, Waziri wa Uchumi na Fedha wa India alisisitiza kwamba, nchi yake haitofuata wala kutekeleza vikwazo visivyo vya kisheria vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuilazimisha New Delhi kuacha kununua mafuta ya nchi hii.