Marekani haina mwamana, yaiwekea vikwazo vingine vipya Korea Kaskazini
Wizara ya Hazina ya Marekani imeweka vikwazo vingine vipya dhidi ya watu na mashirika yenye mfungamano na Korea Kaskazini.
Shirika la habari la Fars limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, Wizara ya Hazina ya Marekani jana Alkhamisi ilitoa taarifa na kusema kuwa, imeliingiza shirika moja lenye makao yake nchini China na shirika jingine lililoko Russia pamoja na mtu mmoja raia wa Korea Kaskazini katika orodha ya vikwazo vyake vipya.
Wizara ya Hazina ya Marekani hivi karibuni pia ilimuwekea vikwazo raia mmoja wa Korea Kaskazini na taasisi tatu za nchi hiyo licha ya Washington na Pyongyang kufikia mapatano ya kuacha uhasama.
Wizara hiyo ya Marekani inadai kuwa uamuzi huo umechukuliwa ili kuzuia kusaidiwa kifedha mradi wa kujiimarisha kwa silaha wa Korea Kaskazini.
Vikwazo vya Marekani dhidi ya Korea Kaskazini vinaendelea licha ya kwamba tarehe 12 Juni mwaka huu, viongozi wa nchi hizo mbili walikutana ana kwa ana nchini Singapore ili kumaliza ugomvi wa mwaka mzima wa kisiasa na kimaneno baina yao.
Rais wa Marekani, Donald Trump na Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un wanadai kuwa wamefikia makubaliano ya kupunguza uhasama baina yao lakini mara kwa mara viongozi wa Pyongyang wanailaumu Marekani kwa kutoheshimu maafikiano hayo.