Ufaransa: Marekani haina haki ya kuchukua maamuzi kwa niaba ya Ulaya
-
Bruno Le Maire
Waziri wa Fedha wa Ufaransa amesema kuwa, Marekani haiwezi kuchukua maamuzi kuhusiana na ushirikiano wa kibiashara wa nchi za Ulaya na Iran na kuongeza kuwa, vikwazo vya serikali ya Washington dhidi ya Iran ni fursa kwa Ulaya kwa ajili ya kuanzisha taasisi zinazojitegemea za kifedha.
Bruno Le Maire ameuambia mkutano unaofanyika huko Slovakia kwamba Umoja wa Ulaya umesasisha sheria ya kukabiliana na vikwazo vya Rais Donald Trump wa Marekani dhidi ya Iran ili kuyawezesha makampuni ya nchi za bara hilo kushirikiana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kibiashara.
Wakati huo huo imepangwa kwamba katika wiki kadhaa zijazo Umoja wa Ulaya utaanza kutekeleza taratibu mpya zitakazodumisha miamala ya kifedha na Iran mkabala wa vikwazo vipya vya kifedha vya Marekani.
Sera za kijuba na kibeberu za Marekani dhidi ya Iran na vitisho vya Rais wa nchi hiyo, Donald Trump vya kuyaadhibu mashirika yanayofanya biashara na Jamhuri ya Kiislamu zimepingwa na hata nchi waitifaki wa serikali ya Washington.
Siku chache zilizopita Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Jean-Claude Juncker alisema kuwa, umewadia wakati kwa nchi za bara hilo kujiamulia mambo yao wenyewe na kuwa huru katika kuchukua maamuzi yanayohusiana na mahusiano ya kimataifa.