NYT: Trump atafeli katika sera zake za vikwazo dhidi ya Iran
Gazeti la New York Times la Marekani limeandika kuwa sera za Rais Trump wa Marekani za kuiwekea vikwazo Iran zitafeli.
Katika makala maalumu iliyoandikwa Jumatano kuhusu duru mpya ya vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran ambavyo vinatazamiwa kuanza Novemba 4, gazeti la New York Times limeandika: "Vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Iran vitakumbwa na changamoto kadhaa mpya na zitafeli maadamu hakuna mabadiliko ya kimsingi ya sera za Trump kuhusu Iran."
New York Times limeashiria matamshi ya Trump kwamba atahakikisha uuzaji mafuta ghafi ya petroli ya Iran duniani unafikia sifuri ifikapo Novemba 4 na kuandika kuwa: "Hivi sasa China na India ambazo ni wanunuzi wakuu wa mafuta ya Iran zinaendelea na ununuzi wao. Uturuki na Russia pia zitafuata mkondo huo kama ambavyo pia Uingereza, Ufaransa na Ujerumani pia zimesema zitaendelea kufanya biashara na Iran."
New York Times limeashiria pia mtazamo wa wanadiplomasia wa Ulaya na wataalamu wa soko la mafuta na kuongeza kuwa: "Hata baada ya kutekelezwa vikwazo vipya vya mafuta dhidi ya Iran, kwa uchache nchi hii itaweza kuuza mapipa milioni moja ya mafuta ghafi ya petroli kwa siku."
Ikumbukwe kuwa mnamo Mei 8, Rais Trump wa Marekani alichukua uamuzi wa upande mmoja wa kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya Iran maarufu kama JCPOA sambamba na kurejesha vikwazo dhidi ya Tehran. Aidha aliapa kuwa ifikapo Novemba 4 2018, atahakikisha kuwa uuzaji mafuta ghafi ya petroli ya Iran katika soko la kimataifa unafikia sifuri. Pamoja na hayo Wizara ya Fedha ya Marekani hivi karibuni imeonekana kulegeza kamba kuhusu vikwazo hivyo na kusema Washington itaziruhusu baadhi ya nchi kuendelea kununua mafuta ya Iran.