Taleban: Hatujahusika na mripuko wa sherehe za Maulidi mjini Kabul, Afghanistan
Msemaji wa kundi la Taleban amekanusha kuhusika kwa aina yoyote kundi hilo katika mripuko wa kigaidi uliotokea kwenye sherehe za maulidi ya Mtume (saw) huko Kabul, mji mkuu wa nchi hiyo.
Zabiullah Mujahid ameyasema hayo Jumatano ya leo na kuongeza kwamba kundi la Taleban halijahusika na shambulizi dhidi ya raia na viongozi wa kidini nchini humo. Jana jioni kulitokea mripuko wa kigaidi katika ukumbi wa hoteli ya Uranus mjini Kabul, wakati idadi kubwa ya Waislamu na wapenzi wa Mtume Muhammad SAW walipokuwa wamekusanyika kwa ajili ya kuadhimisha maulidi ya mtukufu huyo. Katika hujuma hiyo ya kigaidi, zaidi ya watu 50 waliuawa na zaidi ya wengine 70 kujeruhiwa. Hadi sasa hakuna kundi lililotangaza kuhusika na shambulizi hilo, ingawa kwa mara kadhaa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) limekuwa likitangaza kuhusika na jinai kama hizo.
Shirika la Habari la Shafaqna la nchini Afghanistan limetangaza kwamba katika shambulizi hilo la jana aliuawa pia Mullah Abdul Salam Zaeef, mmoja wa viongozi wa kundi la Taleban. Hii ni katika hali ambayo duru za karibu na kiongozi huyo wa Taleban zimedai kwamba Mullah Abdul Salam Zaeef hakuuawa katika mripuko huo. Tayari nchi mbalimbali hasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Uturuki na Pakistan, zimelaani shambulizi hilo la kinyama ambalo linalenga kuchochea moto wa fitina za kidini na kimadhehebu nchini Afghanistan.