Sharti 'lisilo la kawaida' la India la kufanya mazungumzo na Pakistan
Mkuu wa majeshi ya India ameitaka Pakistan iwe na utawala wa kisekula kama sharti la New Delhi kufanya mazungumzo ya amani na kupanua ushirikiano wake na Islamabad.
Jenerali Bipin Rawat amesema hayo katika jibu kwa ujumbe wa hivi karibuni wa amani wa Imran Ahmed Khan Waziri Mkuu wa Pakistan alioutuma kwa India na kusema kuwa, kama Pakistan itakuwa na mfumo wa kisekula kama ilivyo India, basi wakati huo itapata fursa ya kufanya mazungumzo ya amani na nchi yake. Sharti hilo la jenerali huyo wa kijeshi wa India linaweza kutathminiwa katika nukta na pande kadhaa. Mosi ni kuwa, wanajeshi nchini India hawaingilii na kujihusisha na masuala ya kisiasa ya ndani na nje ya nchi hiyo. Kwa kuzingatia sharti lililotolewa na Jenerali Bipin Rawat kwa ajili ya kuanza mazungumzo ya amani ya India na Pakistan inaonesha kufunguliwa ukurasa mpya katika masuala ya utawala nchini India, ambapo sasa wanajeshi wanaonekana kuwa na uwezo wa kuwa na taathira katika siasa za kieneo za New Delhi.
Mwenendo huu ulianza kushuhudiwa tangu mwaka 2014 wakati chama cha Bharatiya Janata kilipoingia madarakani na kushika hatamu za uongozi wa India na hivi sasa mwenendo huo unaonekana kufikia kileleni ambapo taathira zake zimedhihirika zaidi katika mgogoro wa Kashmir. Rashmi Soda Pori, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Punjab nchini India anasema kuwa:
Kadhia ya Kashmir ni moja ya mizozo mikongwe katika historia ya uhusiano wa India na Pakistan na kwamba, kushuhudiwa machafuko ya miongo kadhaa katika eneo hilo ni ishara ya wazi ya kutokuweko azma na irada ya kweli na ya lazima kwa ajili ya kuupatia ufumbuzi mgogoro huo, kiasi kwamba, katika kipindi cha miaka yote hii, hakujakuweko na uungaji mkono wa kutosha kutoka kwa nchi zote mbili katika uwanja huu. Hivi sasa kwa kuweko uingiliaji wa kijeshi, mgogoro huo utazidi kuwa tata.
Jambo la pili la kuzingatiwa kuhusiana na takwa la Mkuu wa majeshi ya India la kuitaka Pakistan iwe na utawala wa kisekula kwanza ili iweze kufanya nayo mazungumzo ya amani, linaonyesha wazi kwamba, jenerali huyo wa kijeshi hana ufahamu kamili na wa kutosha wa Katiba ya Pakistan. Kwa mujibu wa Katiba ya Pakistan ni kuwa, nchi hiyo ina mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na takwa la Bipin Rawat maana yake ni kubadilishwa Katiba ya nchi hiyo jirani na kisha kuundwa mfumo na utawala wa kisekula. Bila shaka kutolewa takwa kama hilo, ni uingiliaji wa wazi katika masuala ya ndani ya Pakistan.
Nukta ya tatu ambayo inapaswa kuzingatiwa pia kuhusiana na sharti la Jenerali Bipin Rawat ni kutupa mpira katika uwanja wa Pakistan sambamba na kutoa tuhuma za kukaririwa kwamba, Islamabad inaunga mkono ugaidi. Kuzungumziwa daima jambo hilo hasa katika miaka ya hivi karibuni, kumeifanya India na Pakistan kushindwa kulisukuma mbele gurudumu la mwenendo wa mazungumzo baina yao. Na ndio maana, uhusiano baina ya nchi mbili hizi ungali unakabiliwa na mgogoro na mvutano.
Kuhusiana na hilo, hatupaswi kupuuza nafasi ya madola ya Magharibi hususan Uingereza katika kuchochea moto wa hitilafu na migogoro katika eneo hususan katika uhusiano wa India na Pakistan.
Alaa kulli haal, hatua ya jenerali Bipin Rawat, kuu wa majeshi ya India ya kuweka sharti la kuweko mfumo wa kisekula kwanza nchini Pakistan ili nchi yake ifanye mazungumzo ya amani na jirani yake huyo, inaonyesha kuwa, wanajeshi wenye misimamo mikali nchini humo ndicho kikwazo kikuu cha kupatiwa ufumbuzi hitilafu na mivutano iliyopo baina ya Islamabad na New Delhi hususan kuhusiana na mzozo wa Kashmir.
Tajiriba ya huko nyuma inaonyesha kuwa, kila mara upande mmoja kati ya pande mbili hizo unapolegeza kamba na kuonyesha utayari wa kufanya mazungumzo na upande wa pili, wanajeshi huko India na Pakistan hujitokeza na kuanza kupiga ngoma ya hitilafu mbalimbali kama vile kuchochea ukosefu wa amani na mizozo zaidi na hivyo kuzizuia Islamabad na New Delhi kupiga hatua kuelekea upande wa mazungumzo ya amani.