Khashoggi na waandishi habari wengine, Watu Mashuhuri mwaka huu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i50108-khashoggi_na_waandishi_habari_wengine_watu_mashuhuri_mwaka_huu
Jarida la kila wiki la Marekani la Time limemteua mwandishi habari na mkosoaji wa utawala wa Saudi Arabia Jamal Khashoggi kuwa ndiye Mtu Mashuhuri wa Mwaka huu (Person of the Year) wa jarida hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 11, 2018 21:40 UTC
  • Khashoggi na waandishi habari wengine, Watu Mashuhuri mwaka huu

Jarida la kila wiki la Marekani la Time limemteua mwandishi habari na mkosoaji wa utawala wa Saudi Arabia Jamal Khashoggi kuwa ndiye Mtu Mashuhuri wa Mwaka huu (Person of the Year) wa jarida hilo.

Time pia limewateua waandishi wengine kadhaa pamoja na Khashoggi ambao limesema wamestahiki nafasi hiyo kutokana na kujitolea kwao katika "vita vya kufichua uhakika".

Jarida la Time limeandika kuwa, bwana huyo jasiri amethubutu kuhitilafiana na utawala wa nchi yake na kuipasha dunia habari kuhusu ukatili wa watawala wa Riyadh dhidi ya watu wanaopaza juu sauti zao na akauawa katika njia hiyo.

Jarida hilo limeongeza kuwa, Jamal Khashoggi ameanika ukweli na uhakika kuhusu Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia na utovu wa maadili wa muungano wa Saudia na Marekani.

Ripoti ya shirika la ujasusi la Marekani (CIA) imethibitisha kuwa, Jamal Khashoggi aliuliwa kwa amri ya moja kwa moja iliyotolewa na Muhammad bin Salman, lakini serikali ya Washington hadi sasa imekwepa kuichukulia hatua Saudia ili kulinda mikataba ya mabilioni ya dola ya mauzo ya silaha kwa utawala huo wa kifalme.

Baada ya kuuliwa maiti ya Khashoggi ilikatwa vipande vipande na kupelekwa kusikojulikana.