Trump hamsazi yeyote, azishambulia vikali Facebook, Twitter na Google
Sanjari na kuendelea kuwashambulia wakosoaji wake na hata kuwafukuza kazi wapambe wake, rais wa Marekani Donald Trump sasa ameelekeza makombora yake dhidi ya mashirika ya intaneti na mitandao ya kijamii ya Google, Facebook na Twitter.
Katika ujumbe alioutuma kwenye ukurasa wake wa Twitter hapo jana, Trump ameandika, "Facebook, Twitter na Google zinawapendelea Wademokrat, ni masikhara! Twitter imetia ugumu kwa watu kufuata ukurasa wangu na pia wamefuta akaunti nyingi."
Trump hivi karibuni pia alitumia mtandao huo wa kijamii anaoushambulia wa Twitter kusema kuwa, "Hatua ya Twitter ya kuwapiga marufuku shakhsia mashuhuri wa Republican si jambo zuri, tutafuatilia suala hili la kibaguzi na ambalo liko kinyume cha sheria. Watu wengi wanalalamika."
Licha ya kuishambulia vikali Twitter, lakini rais huyo wa Marekani amekuwa akiutumia mtandao huo wa kijamii kama jukwaa lake kuu la kutoa taarifa rasmi na zisizo rasmi, na hata kuwakebehi na kuwakejeli wapinzani na wakosoaji wake.
Siku chache zilizopita, wawakilishi wa chama wa Republican walimjia juu Ofisa Mkuu Mtendaji wa shirika la Intaneti la Google, na kumtaka afafanue kwa nini kila mara mtu anapotafuta neno 'mpumbavu' kwenye mtandao huo, picha zinazokuja ni za Donald Trump.