"Mbwa Kichaa" ajiuzulu, sababu ni hitilafu kati yake na Donald Trump
Waziri wa Ulinzi wa Marekani James Mattis maarufu kwa jina la "Mbwa Kichaa" amejiuzulu wadhifa huo kutokana na hitilafu za kimitazamo kati yake na Rais Donald Trump wa hiyo.
Mattis ambaye ni jenerali mstaafu ataachia ngazi mwishoni mwa mwezi Februari na kumruhusu Rais Trump kuchagua mtu anayekwenda sambamba na mitazamo yake.
Jenerali Mattis amesema katika barua yake ya kujiuzulu kwamba, hatua hiyo itampa Trump fursa ya kumteua mtu anayeoana zaidi ya mitazamo na fikra zake.
Kujiuzulu kwa Mbwa Kichaa au Mad Dog kama anavyojulikana kulitazamiwa hususan baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kutangaza Jumatano iliyopita kwamba, ataliondoa jeshi la nchi hiyo nchini Syria.
James Mattis anajiunga katika orodha ndefu ya maafisa wa ngazi za juu serikali ya Trump ama waliojiengua wao wenyewe au kufukuzwa kazi kama waziri wa zamani wa mambo ya nje wa nchi hiyo, Rex Tillerson ambaye alitumuliwa na Donad Trump kupitia ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter.
Uchunguzi wa kituo cha Brookings Institution unasema serikali ya Trump imetimua idadi kubwa zaidi ya maafisa wake kuliko serikali za marais watano wa kabla yake.