Wamarekani waliowengi wanapinga ujenzi wa ukuta mpakani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i50683-wamarekani_waliowengi_wanapinga_ujenzi_wa_ukuta_mpakani
Uchunguzi mpya wa maoni umebiani kuwa wananchi waliowengi Marekani wanapinga mpango wa Rais Donald Trump wa nchi hiyo wa kujenga ukuta katika mpaka wa nchi hiyo na Mexico.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 06, 2019 10:36 UTC
  • Wamarekani waliowengi wanapinga ujenzi wa ukuta mpakani

Uchunguzi mpya wa maoni umebiani kuwa wananchi waliowengi Marekani wanapinga mpango wa Rais Donald Trump wa nchi hiyo wa kujenga ukuta katika mpaka wa nchi hiyo na Mexico.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni wa pamoja uliofanywa na na mashirika ya  Harvard CAPS na Harris na kuchapishwa Jumapili, asilimia 66 ya Wamarekani wanapinga mpango wa Donald Trump wa kujenga ukuta katika mpaka wa Marekani na Mexico.

Uchunguzi huo wa maoni umebaini kuwa asilimia 31 ya Marekani wanasema ujenzi wa ukuta huo si dharura na utagharimu kiasi kikubwa cha fedha huku wengine asilimai 31 wakisema kunaweza kutumika njia bora zaidi za kudhamini usalama mpakani.

Trump analishinikiza Baraza la Congress limpe mabilioni ya dola za kujengea ukuta huo, lakini chama cha Democrats kinasema kuwa, hakiwezi kuruhusu baraza hilo litenge fedha za kuendeshea mradi wa "kipuuzi" kama huo hasa kwa vile Trump aliwaahidi wapiga kura kuwa Wamexico ndio watakaogharamia ujenzi wa ukuta huo. Mzozo umekuwa mkubwa hivi sasa kiasi kwamba Trump ameamua kufunga taasisi za serikali tangu tarehe 22 Disemba 2018 hadi leo hii.

Sehemu ya Ukuta katika mpaka wa Mexico na Marekani

Trump anahitajia bajeti ya dola bilioni 5 na milioni 600 za kujengea ukuta huo. Anadai kuwa, ukuta huo utasaidia sana kupambana na wimbi la wahajiri wanaoingia nchini Marekani kinyume cha sheria kupitia Mexico. Juzi Alkhamisi, Trump alisema mbele ya waandishi wa habari katika Ikulu ya Marekani, White House, kwamba nchi hiyo haiwezi kuwa na amani kama hakutajengwa ukuta katika mpaka wake na Mexico.