Kiongozi wa Wademocrati akataa pendekezo jipya la Trump
Kiongozi wa wawakilishi wa chama cha Democratic katika Baraza la Seneti la Marekani amekataa pendekezo la Rais Donald Trump wa nchi hiyo kwa ajili ya kukomesha hatua yake ya kufunga shughuli zote za serikali ya nchi hiyo.
Kiongozi wa Wademocrati katika Seneti ya Marekani, Chuck Schumer ameandika katika ukurasa wa mtandao wa Twitter kwamba Donald Trump amejiweka yeye na serikali katika hali isiyokubalika kwa kufunga shughuli za serikali.
Chuck Schumer ameongeza kuwa, Trump mwenyewe ndiye aliyeamua kufuta sheria ya DACA na pendekezo la kurejesha sheria hiyo mkabala wa kupewa bajeti ya kujenga ukuta katika mpaka wa Marekani na Mexico siyo suluhishi bali ni aina fulani ya kuwashikilia mateka raia wa Marekani.
Jumamosi ya Jana Rais Donald Trump alitoa pendekezo la kuwapa vibali halali vya kuishi Marekani maelfu ya wahajiri mkabala wa Kongresi kuipatia serikali yake bajeti ya kujenga ukuta katika mpaka wa nchi hiyo na Mexico; suala ambalo limepingwa na Wademokrati.
Shetia ya DACA ilianza kutekelezwa mwaka 2010 kwa amri ya aliyekuwa rais wa Marekani Barack Obama. Sheria hiyo inawaruhusu watoto wa wahajiri wasio na vibali vya kuishi Marekani waliokulia nchini humo kuendelea kuishi Marekani hadi pale watakapokamilisha masharti ya kupewa uraia. Serikali ya Trump imefuta sheria hiyo ya DACA.