Misala ya Waislamu yamtia kiwewe rais wa Marekani, Donald Trump
Njama mpya za rais wa Marekani, Donald Trump za kujaribu kuchafua sura ya Waislamu na wahajiri wanaoingia nchini humo, zimeonesha ni kiasi gani rais huyo alivyo na mtazamo finyu kuhusiana na Uislamu na jinsi anavyotiwa kiwewe na dini hiyo ya Mwenyezi Mungu.
Siku ya Ijumaa, Trump aliandika katika ukurasa wa kijamii wa Twitter kwamba eti kumepatikana misala katika mizigo ya wahajiri kwenye mpaka wa Marekani na Mexico.
Wanaharakati wa Kiislamu wamelaani vikali njama hizo mpya za Trump dhidi ya Waislamu na wahajiri na wameamua kuanzisha kampeni maalumu ya "Msala Wangu" katika mitandao ya kijamii.
Ujumbe huo wa Twitter wa Trump umeenea sana kati ya Waislamu wa Marekani ambao wamelaani vikali madai yake hayo na kusema kuwa, huo ni mfano wa wazi wa chuki zake dhidi ya Waislamu na ubaguzi wake mkubwa.
Ahmad Rahab, mkuu wa Baraza la Uhusiano wa Marekani na Uislamu tawi cha Chicago ameanzisha kampeni maalumu ya Hashtag ya "My Prayer Rug" na kuandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba kuwa Muislamu ni uhalifu na kosa kwa mtazamo wa rais wa Marekani.
Amesema, Trump anajaribu kuwatisha wananchi wa Marekani kwa kudai kuwa eti Waislamu wanaingia kinyume cha sheria nchini humo.
Donald Trump ni maarufu kwa chuki zake dhidi ya wahajiri hasa Waislamu kiasi kwamba aliwahi kusema katika kampeni zake za uchaguzi kwamba, akichaguliwa kuwa rais wa Marekani, atapiga marufuku Waislamu kuingia nchini humo.