Bangladesh yawazuia kuingia nchini humo Waislamu 31 wa Rohingya waliokimbia India
(last modified Tue, 22 Jan 2019 02:46:50 GMT )
Jan 22, 2019 02:46 UTC
  • Bangladesh yawazuia kuingia nchini humo Waislamu 31 wa Rohingya waliokimbia India

Bangladesh imektaa kuwapokea makumi ya Waislamu wa JAMII YA Rohingya waliotaka kuingia nchini humo wakitokea nchi jirani ya India; na hivyo kuwaacha raia hao wakiwa wamekwama katika eneo lisilo na makazi kwenye mpaka wa nchi hizo mbili.

Golam Kabir, kamanda wa walinzi wa mpakani wa Bangladesh amesema kuwa kundi hilo la Waislamu wa Rohingya lenye wanawake na watoto 31 limekwama katika eneo hilo la mpaka wa Bangladesh na India tangu siku ya Ijumaa. Ameongeza kuwa waliwazuia Waislamu hao wa Rohinga kuingia Bangladesh wakati wakijaribu kuvuka mpaka na kwamba duru mbili za mazungumzo zilichofanyika kati yao na kikosi cha ulinzi wa mpakani cha India kuhusu hadhi ya kisheria ya raia hao zimegonga mwamba.

Makazi ya Waislamu wa Rohingya yakiwa yamechomwa moto mkoani Rakhine nchini Myanmar

Jeshi la Myanmar limezidisha mashambulizi na vitendo vya ukandamizaji dhidi ya Waislamu wa Rohingya tangu mwaka 2017 hususan dhidi ya wale wanaoishi katika mkoa wa Rakhine wa magharibi mwa nchi hiyo ambao wanauliwa ovyo na mabudha na wanajeshi wa Myanmar na nyumba zao kuchomwa moto.

Wakati huo huo Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limesema kuwa, limesajili wakimbizi wa jamii ya Rohingya wasiopungua 16,500 huko India hata hivyo India haitambui kadi hizo za UNHCR.