Uturuki kupeleka kadhia ya mauaji ya Khashoggi katika Umoja wa Mataifa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki amesema kuwa umewadia wakati wa kufanyika uchunguzi wa kimataiifa kuhusu mauaji ya mwandishi habari na mkosoaji wa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia, Jamal Khashoggi.
Mevlüt Çavuşoğlu amesema kuwa Rais Recep Tayyep Erdogan wa Uturuki ameamuru kadhia hiyo ihamishiwe katika ngazi ya kimataifa.
Amesema Rais Erdogan ametaka kuchukuliwe hatua za lazima za kuwasilisha kadhia ya mauaji ya Khashoggi katika ngazi za kimataifa na kwamba ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa atawasili Uturuki Jumapili ijayo kwa ajili ya suala hilo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki amesema kuwa umewadia wakati wa kufanyika uchunguzi wa kimataifa katika mauaji ya mkosoaji huyo wa utawala wa Saudia na kwamba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linapaswa kutoa kibali cha kufanyika uchunguzi huo. Hata hivyo Mevlüt Çavuşoğlu amesema, kuna uwezekano kwamba baraza hilo halitaweza kutoa kibali hicho, hivyo chaguo jingine ni kuundwa tume ya kimataifa itakayoundwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa au Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa umoja huo kusimamia uchunguzi huo.
Ushahidi na nyaraka zote zilizopo, zikiwemo taarifa zilizotolewa na serikali ya Uturuki na Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) zinaonyesha kuwa Muhammad bin Salman, mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia ndiye aliyekuwa mpangaji mkuu wa jinai ya kutisha na mauaji ya Jamal Khashoggi.
Jamal Khashoggi, aliyewahi kuwa msiri na mwandani wa familia ya kifalme inayotawala nchini Saudi Arabia, aliuliwa na maafisa wa utawala huo na mwili wake kukatwa vipande vipande baada ya kuingia kwenye jengo la ubalozi mdogo wa nchi hiyo mjini Istanbul, Uturuki mnamo tarehe Pili Oktoba mwaka uliopita.