Mbunge Mwislamu wa Marekani aunga mkono kuundwa dola huru la Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/world-i51419-mbunge_mwislamu_wa_marekani_aunga_mkono_kuundwa_dola_huru_la_palestina
Mbunge Mwislamu katika Bunge la Marekani anayetoka katika chama cha Demokrat ametoa wito wa kuchukuliwa misimamo imara zaidi kuhusiana na eneo la Mashariki ya Kati hususan kuundwa kwa dola huru la Palestina.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 08, 2019 10:49 UTC
  • Mbunge Mwislamu wa Marekani aunga mkono kuundwa dola huru la Palestina

Mbunge Mwislamu katika Bunge la Marekani anayetoka katika chama cha Demokrat ametoa wito wa kuchukuliwa misimamo imara zaidi kuhusiana na eneo la Mashariki ya Kati hususan kuundwa kwa dola huru la Palestina.

Bi Ilhan Omar amesema yeye pamoja na mbunge mwenzake mwingine Mwislamu Rashida Tlaib watahakikisha wanakilazimisha chama chao kichukue misimamo imara zaidi kuhusiana na matukio ya eneo la Mashariki ya Kati hususan kadhia ya kuundwa dola huru la Palestina.

Aidha akizungumza katika kamati ya masuala ya kigeni ya Bunge la Marekani hapo jana, Bi Ilhan Omar mwenye asili ya Somalia aliitaka serikali ya Saudi Arabia ilipe umuhimu suala la haki za binadamu na kuliweka suala hilo katika kiwango sawa na cha mataifa mengine yanayoheshimu haki za binadamu.

Kadhalika Mbunge huyo wa kwanza mwanamke Mwislamu katika Kongresi ya Marekani hivi karibuni alitoa wito wa kusitishwa uuzaji wa silaha kwa utawala wa Saudi Arabia. 

Kutokana na misimamo yake hiyo imara ya kupinga ukandamizaji unaofanywa na Saudi Arabia, mbunge Ilhan Omar wa Kongresi ya Marekani amekuwa akishambuliwa mara kwa mara na vyombo vya habari vya serikali ya Riyadh. 

Mashirika na jumuiya za kimataifa za kutetea haki za binadamu zimekuwa zikitoa wito wa kusitishwa uuzaji wa silaha za nchi hiyo kwa utawala wa kiimla wa Saudi Arabia kutokana na mauaji yanayofanywa na utawala wa Riyadh dhidi ya watu wasio na hatia wa Yemen hususan wanawake na watoto wadogo.