Seneta wa Marekani asema huenda Trump 'atafungwa jela' kufikia 2020
https://parstoday.ir/sw/news/world-i51475-seneta_wa_marekani_asema_huenda_trump_'atafungwa_jela'_kufikia_2020
Seneta wa chama cha Democrats nchini Marekani amesema yumkini Rais Donald Trump wa nchi hiyo atakuwa gerezani kabla ya uchaguzi mkuu ujao nchini humo mwaka ujao 2020.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 11, 2019 04:17 UTC
  • Seneta wa Marekani asema huenda Trump 'atafungwa jela' kufikia 2020

Seneta wa chama cha Democrats nchini Marekani amesema yumkini Rais Donald Trump wa nchi hiyo atakuwa gerezani kabla ya uchaguzi mkuu ujao nchini humo mwaka ujao 2020.

Seneta huyo wa upinzani, Elizabeth Warren na ambaye ametangaza azma yake ya kugombea kiti cha rais katika uchaguzi ujao nchini humo alisema hayo jana Jumapili akiwa katika mkutano wa kampeni mjini Cedar Rapids, jimboni Iowa.

Huku akiashiria uchunguzi unaoendelea hivi sasa kuhusu uhusiano wa Marekani na Russia, Seneta huyo amebainisha kuwa, "kinachotia wasiwasi ni kuwa, kufikia mwaka 2020, Trump sio tu hatakuwa rais wa nchi, bali pia huenda asiwe mtu huru." 

Mwanasiasa huyo wa Democrats amemtaja Trump kuwa matokeo ya mfumo uliochakachuliwa na anayetumikia maslahi ya matajiri walio wachache na watu wenye ushawishi, huku akiwapaka matope watu wengine wote. 

Trump amekuwa akikosolewa na wapinzani na hata wapambe wake wakiwemo wanachama wa chama tawala cha Republican.

Rais Donald Trump wa Marekani

Utafiti wa maoni uliofanywa na shirika la habari la CNBC hivi karibuni unaonesha kuwa Trump anaendelea kupoteza uungaji mkono sio tu miongoni mwa wananchi, bali pia miongoni mwa wafanyabiashara tajiri waliomuunga mkono katika kampeni zake za uchaguzi uliopita mwaka 2016.

Kwa mujibu wa utafiti huo, ni asilimia 34 tu ya mamilionea nchini Marekani ndio wameonesha kuwa watamuunga mkono Trump katika uchaguzi ujao wa rais wa mwaka 2020, ikilinganishwa na asilimia 45 mwaka jana.