Mbunge wa Democrats: Trump ndiye tishio kuu kwa demokrasia ya Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i51773-mbunge_wa_democrats_trump_ndiye_tishio_kuu_kwa_demokrasia_ya_marekani
Mwakilishi wa chama cha upinzani cha Democrats amesema Rais Donald Trump ndiye tishio nambari moja kwa demokrasia ya Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 25, 2019 00:49 UTC
  • Mbunge wa Democrats: Trump ndiye tishio kuu kwa demokrasia ya Marekani

Mwakilishi wa chama cha upinzani cha Democrats amesema Rais Donald Trump ndiye tishio nambari moja kwa demokrasia ya Marekani.

Jerrold Nadler, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria ya Kongresi ya Marekani amesema, "Namtazama huyu rais na mienendo yake kama tishio kuu kwa mfumo wa demokrasia na utawala wa kikatiba hapa Marekani, tangu baada ya vita vya ndani."

Amemkosoa vikali Trump kwa kutoa kauli za vitisho na kejeli dhidi ya vyombo vya habari na mihimili ya serikali kama vile idara ya mahakama.

Mwakilishi huyo ambaye ana mamlaka ya kuagiza uchunguzi juu ya mienendo ya Trump amedokeza kuwa, "Kongresi itaitisha vikao vya kujadili mambo kadhaa, ikiwemo hatua ya Trump ya kutumia vibaya mamlaka pamoja na kuzuia au kupindisha mkondo wa sheria."

Rais Donald Trump

Mienendo hasi ya Trump imekuwa ikikosolewa na wanachama wa Democrats na pia wanasiasa wa chama tawala cha Republican.

Kadhalika wananchi wa Marekani wamekuwa wakifanya maandamano mara kwa mara kupinga misimamo na sera za Trump; maandamano ya hivi karibuni yakiwa yale ya kupinga uamuzi wa rais huyo wa kutangaza hali ya hatari kwa ajili ya kushinikiza kupewa bajeti ya ujenzi wa ukuta katika mpaka wa nchi hiyo na Mexico.