Mafuriko yaua watu 45 Afghanistan na Pakistan
Kwa akali watu 45 wamepoteza maisha kutokana na mafuriko makubwa yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika nchi za Afghanistan na Pakistan.
Ofisi ya Uratibu ya Umoja wa Mataifa Inayoshughulikia Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imetangaza kuwa, watu 25 wamepoteza maisha katika sehemu mbalimbali za Pakistan kutokana na mafuriko hayo.
Taarifa ya OCHA imesema kuwa, watu tisa wameaga dunia katika maeneo ya kikabila nchini humo, watatu katika mkoa wa Khyber Pakhtunkhwa huku 13 wakisombwa na maji na kuaga dunia katika mkoa wa Balochistan.
Waziri wa Habari wa Balochistan, Zahoor Ahmed Buledi amesema mbali na watu 13 kuaga dunia katika mkoa huo, wengine 12 wamejeruhiwa.
Habari zaidi zinasema kuwa, watu zaidi ya 20 wamepoteza maisha katika mafuriko hayo hususan katika mkoa wa Kandahar, huku nyumba zaidi ya elfu moja zikisombwa na mafuriko hayo.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, watu 52 wamefariki dunia kutokana na mafuriko nchini Afghanistan, tokea Februari 12 hadi sasa.