Mar 23, 2019 13:53 UTC
  • Wamarekani weusi waandamana kupinga kitendo cha kufutiwa mashtaka polisi mzungu aliyeua kijana mweusi

Wanasheria na familia ya kijana mwenye asili ya Kiafrika aliyeuawa na polisi mzungu nchini Marekani wamefanya maandamano mbele ya mahakama wakilaani kitendo cha kufutiwa mashtaka polisi huyo muuaji katika jimbo la Pennsylvania.

Maandamano hayo yamefanyika ikiwa ni baada ya kamati ya usawa ya mahakama ya mji wa Pittsburgh katika jimbo la Pennsylvania kumfutia tuhuma afisa wa zamani wa polisi kwa jina la Michael Rosfeld, aliyemuua bila ya hatia kijana mwenye asili ya Kiafrika aliyetambuliwa kwa jina la Antwon Rose. Kwa mujibu habari hiyo, Rosfeld aliyempiga risasi Antwon aliyekuwa na umri wa miaka 17 kwa nyuma, alifutiwa tuhuma dhidi yake Ijumaa ya jana hukumu ambayo imewakasirisha mno watetezi wa haki za binaadamu na familia pamoja na watu wa familia ya kijana huyo.

Kijana Antwon Rose kushoto aliyeuawa, na kulia ni Michael Rosfeld, polisi mzungu muuaji

Inaelezwa kwamba afisa huyo wa polisi alitenda jinai hiyo mwezi Juni mwaka jana na kwamba kijana huyo aliyeuawa alikuwa hana silaha yoyote. Ukweli ni kwamba mauaji dhidi ya Antwon Rose ni sehemu ndogo ya jinai na mauaji chungu nzima yanayofanywa na polisi wazungu kuwalenga vijana wenye asili ya Kiafrika nchini Marekani. Mwezi Februari mwaka huu pia mwendesha mashtaka wa jimbo la California aliwaachia huru polisi wawili waliohusika kumuua kijana mwingine mwenye asili ya Afrika katika mji wa Sacramento wa la California. Mienendo hiyo isiyo ya kiuadilifu ya polisi na vyombo vya mahkama nchini Marekani dhidi ya jamii Wamarekani weusi, imekuwa ikilalamikiwa vikali katika maeneo tofauti ya nchi hiyo inayojidai kuwa mtetezi wa haki za binaadamu duniani.

Tags