Apr 04, 2019 02:38 UTC
  • Brunei yaanza kutumia sheria za Kiislamu kuwaadhibu wazinzi na mashoga

Jamhuri ya Brunei jana Jumatano ilianza kutekeleza awamu ya pili ya sheria za Kiislamu katika adhabu ya makosa ya jinai nchini humo.

Mfalme wa Brunei Hassanal Bolkiah ameidhinisha kuanza kutekelezwa sheria hizo katika nchi hiyo ndogo ya kusini mashariki mwa bara la Asia. Kwa mujibu wa sheria hiyo, watakaopatikana na hatia katika mashitaka ya kufanya uzinzi, ubaradhuli, kuvunjia heshima Qur’ani Tukufu na Mtume Mtukufu Muhammad (SAW), watakahukumiwa adhabu ya kupigwa mawe hadi kufa.

Aidha katika sheria hiyo iliyoanza kutekelezwa jana Jumatano, atakayepatikana na hatia ya kuiba atakatwa mkono wa kulia ikiwa amefanya kosa hilo kwa mara ya kwanza, na mkono wa kushoto iwapo atapatikana na hatia ya wizi kwa mara ya pili. 

Brunei ambayo ina watu karibu 430,000 imeanza kutekeleza sheria hizo za Kiislamu licha ya Marekani, Uingereza, Ujerumani, Ufaransa na nchi nyingine za Magharibi kuitaka isitekeleze awamu ya pili ya sheria hizo.

Uamuzi huo wa Brunei umezighadhabisha nchi za Magharibi

Awamu ya kwanza ya sheria hizo ilianza kutumika Mei mwaka 2014, ambapo wananchi wa nchi hiyo ya Kiislamu walianza kufikishwa kortini na kupigwa faini au kufungwa kwa kutenda makosa kama vile kubeba mimba nje ya ndoa, kushindwa kuhudhuria Sala ya Ijumaa na kuhubiri dini nyingine isiyo ya Kiislamu.

Mabadiliko hayo yanaungwa mkono na aghalabu ya wananchi wa nchi hiyo ambao karibu wote ni Waislamu.

Tags