Ripoti: Chuki dhidi ya Waisraeli yaongezeka maradufu nchini Marekani
Ripoti mpya inaonesha kuwa mashambulizi na matamshi ya chuki dhidi ya Mayahudi wanaoishi nchini Marekani yameongezeka maradufu.
Kwa mujibu wa jumuiya ya Anti-Defamation League (ADL), visa vya chuki dhidi ya watu wenye asili ya utawala wa Kizayuni wa Israel nchini Marekani vilivyorekodiwa mwaka jana 2018 ni 1,879, ikilinganishwa na 979 mwaka 2017.
Jonathan Greenblatt, Afisa Mkuu Mtendaji wa ADL amesema Mayahudi 59 waliuawa katika hujuma za moja kwa moja dhidi yao au taasisi za Kiyahudi mwaka jana 2018 nchini Marekani, hilo likiwa ni ongezeko la asilimia 105 ikilinganishwa na mwaka juzi.
Huku akishiria shambulio dhidi ya Sinagogi la Mayahudi katika mji wa Poway karibu na jimbo la Carlifornia Jumamosi iliyopita ambapo Myahudi mmoja aliuawa kwa kupigwa risasi, Greenblatt amesema mashambulio yanayotokana na chuki dhidi ya Mayahudi yanaonekana kushtadi mno nchini humo mwaka huu 2019.
Haya yanajiri miezi miwili baada ya serikali ya Ufaransa kusema kuwa vitendo na matamshi ya chuki dhidi ya Mayahudi wanaoishi katika nchi hiyo ya Ulaya yameongezeka kwa asilimia 74, rekodi ambayo haijawahi kushuhudiwa tena.
Ufaransa inatajwa kuwa nchi yenye idadi kubwa zaidi ya wahamiaji wa Kiyahudi baada ya Marekani. Utawala ghasibu wa Israel hivi sasa unaendelea kupora na kukalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina, mbali ya kuwafanyia kila aina ya ukatili.