Jun 03, 2019 04:29 UTC
  • Ufyatuaji risasi wajiri mbele ya ikulu ya Marekani White House

Vyombo vya habari nchini Marekani vimeripoti kujiri ufyatuaji risasi mbele ya ikulu ya nchi hiyo White House.

Kwa mujibu wa habari hiyo, maafisa usalama wa Marekani wamemfyatulia risasi mtu mmoja mbele ya ikulu ya White House wakati akijaribuu kuingia ikulu hiyo. Aidha habari hizo zimeongeza kwamba mtu huyo aliingia eneo lililopigwa marufuku watu kuingia upande wa kaskazini mwa ikulu hiyo, ikiwa ni muda mfupi baada ya Rais Donald Trump kuelekea nje ya nchi. Inaelezwa kwamba kabla ya maafisa usalama wa siri wa Marekani kumfyatulia risasi mtu huyo walianza kumuonya. Hadi sasa vyombo vya habari havijaweza kufahamu utambulisho wa mtu huyo na lengo lake la kutaka kuingia White House. Hayo yanajiri katika hali ambayo, hivi karibuni pia mtu mmoja aliyekuwa akitembea kwa miguu mjini Washington alifika mbele ya ikulu hiyo ya Rais Donald Trump na kujimwagia mafuta na kisha kujichoma moto, akilalamikia hali ngumu ya maisha. 

Mvutano kati ya Nancy Pelosi, Spika wa Bunge la Wawakilishi la Marekani na Trump

Katika hatua nyingine Nancy Pelosi, Spika wa Bunge la Wawakilishi la Marekani amesisitiza kwamba ni lazima Rais Donald Trump wa nchi hiyo ahojiwe katika kongresi na mahkama ya Marekani kutokana na hatua zake zenye utata. Pelosi ameyasema hayo akihutubia mkutano wa kila mwaka wa chama cha Democrat katika jimbo la California ambapo akiashiria juu ya ripoti ya mwisho ya Robert Mueller, mchunguzi maalumu wa faili la madai ya uingiliaji wa Russia katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2016 nchini Marekani, ameongeza kwamba katika ripoti hiyo Mueller ameonya wazi kwamba kulifanyika hujuma kwenye uchaguzi na demokrasia nchini Marekani ingawa hadi sasa Rais Donald Trump anajaribu kutetea hujuma hiyo. Aidha amesema kuwa bunge la Marekani bado linaendelea kumchunguza Trump na serikali yake. 

Tags