Jun 16, 2019 02:16 UTC
  • Moscow yailaumu Marekani kwa kuibua mivutano Asia magharibi

Marekani katika kipindi hiki cha utawala wa Rais Donald Trump imeanzisha jitihada za kuasisi muungano na kuimarisha uwepo wake katika eneo la Asia magharibi hususan katika Ghuba ya Uajemi kwa kisingizio cha eti kuwepo vitisho kutoka kwa Iran.

Hatua hizo za Marekani zimekabiliwa na jibu kali ya Moscow. Baada ya kulipuliwa meli za mafuta katika Bahari ya Oman juzi Alhamisi na kisha serikali ya Trump kuituhumu Iran kuwa ndiyo iliyohusika na milipuko hiyo, Russia imetahadharisha juu ya uwezekano wa kutumiwa tukio hilo kwa ajili ya kuishinikiza Iran na kupanua mivutano. Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia  Ijumaa tarehe 14 Juni ilitoa taarifa ikizitaja siasa na hatua za Marekani dhidi ya Iran kuwa ndiyo sababu ya kushtadi mivutano katika eneo la Asia magharibi ikiwemo katika Bahari ya Oman. Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imetahadharisha kuhusu kutolewa uamuzi wa aina yoyote bila ya ushahidi kuhusu tukio hilo lililojiri katika Bahari ya Oman kabla ya kufanyika uchunguzi wa kimataifa na kusisitiza kuwa, mtu yoyote hapasi  kunyooshewa kidole cha lawama kabla ya kukamilika uchunguzi huo. 

Alkhamisi iliyopita pia ikulu ya Rais wa Russia, Kremlin ilieleza kuwa, ni mapema sana kuweza kutoa uamuzi juu ya nani aliyehusika na shambulio dhidi ya meli mbili za mafuta katika Bahari ya Oman na ikatahadharisha kuhusu kutolewa uamuzi bila ya kuwa na ushahidi wa kutosha. Taarifa ya Kremlin ilitolewa muda mfupi baada ya afisa mmoja wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani kudai kuwa, kuna uwezekano mkubwa Iran imehusika na shambulio dhidi ya meli hizo mbili za mafuta. Baadaye pia viongozi wa ngazi ya juu wa Marekani akiwemo Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa nchi hiyo,  Mike Pompeo walidai kwamba Iran imehusika katika tukio hilo. Rais Donald Trump wa Marekani pia aliibuka na kuwavunjia heshima kwa mara nyingine tena wananchi wa Iran pale alipowataja kuwa ni magaidi bila ya kuonesha nyaraka wala ushahidi wowote wa madai hayo. Trump aliituhumu Iran kuwa imehusika katika kulipua meli mbili za mafuta katika Bahari ya Oman Alhamisi iliyopita.  

Mike Pompeo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani 
 

Siku iliyofuata yaani Ijumaa asubuhi akijibu swali aliloulizwa katika mazungumzo na televisheni ya Fax News kwamba tathmini yenu kuhusu tukio hilo ni nini? Donald Trump alisema: Iran ndiyo iliyofanya shambulizi hilo.  

Licha ya madai ya viongozi wa Marekani kwamba wanafanya jitihada za kuondoa hali ya mivutano katika Ghuba ya Uajemi na kutaka kufanya mazungumzo na Iran lakini kivitendo, serikali ya Trump inataka kuidhihirisha Iran kuwa imehusika na tukio la Bahari ya Oman na matukio mengine ya kuvuruga usalama katika eneo la Mashariki ya Kati na kwa msingi huo Washington iweze kuhalalisha kuiwekea Iran mashinikizo ya kiwango fulani. Kwa kutumia kisingizio na madai hayo pia Washington inataka kuunda muungano wa kimataifa dhidi ya Tehran. Pamoja na hayo yote, hatua hizo za Trump zimegonga mwamba na mbali na waitifaki wa Washington kama Saudi Arabia, Imarati au Uingereza, nchi nyingine zimedhihirisha wazi misimamo yao zikisema kuwa kuna ulazima wa kufanyika uchunguzi zaidi kuhusu tukio la karibuni katika Bahari ya Oman bila ya kuituhumu Iran.  Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Heiko Maas ameashiria video ya Marekani iliyodai kuwa picha hiyo inaonyesha namna boti ya Iran ilivyokaribia katika meli ya mafuta ya Japan na kueleza kuwa: Mkanda wa video uliotolewa na Marekani kuhusu meli hiyo ya Japan hautoshi kupata matokeo kuhusu  nafasi ya Iran katika kushambuliwa meli hizo. Viongozi wa kimataifa pia wamechukua hatua sawa na hiyo ya Ujerumani. Antonio Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelaani shambulio dhidi ya meli hizo za mafuta na kueleza kuwa, uchunguzi huru unapasa kufanyika bila ya kuegemea upande wowote. 

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa UN

Hii ni katika hali ambayo Iran imesisitiza mara kadhaa juu ya ulazima wa kuwepo amani na utulivu katika eneo la Ghuba ya Uajemi na kwamba, inapinga hatua za kuzusha mivutano na ukosefu wa amani za Magharibi hususan zinazotekelezwa na Marekani katika eneo hilo. Iran inafanya kila iwezelalo kuhakikisha kuwa amani na utulivu vinakuwepo katika eneo hilo.

Kuhusiana na suala hilo hivi karibuni Muhammad Javad Zarif Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alitangaza kuwa Tehran iko tayari kusaini makubaliano ya kikanda ya kutoshambuliana. Pamoja na hilo, Washington inafanya kila iwezalo kufanikisha kivitendo malengo iliyoyakusudia ikiwa ni pamoja na kuidhihirisha Iran kuwa ni tishio na kuzidisha mauzo ya silaha kwa waitifaki wake.  Matamshi ya karibuni ya Trump pia yanaonyesha kuwa, licha ya kudai kuwa na hamu ya kufanya mazungumzo na Iran lakini nguzo kuu ya sera zake mkabala wa Iran ni kutoa vitisho, kutumia mabavu na mashinikizo. 

Tags