India yajibu mapigo, yatangaza ushuru wa juu kwa bidhaa za Marekani
Serikali ya India imetangaza ushuru wa juu wa forodha kwa bidhaa 28 za Marekani, ikiwa ni radimali ya nchi hiyo ya Asia kwa vikwazo vya kibiashara vya Washington dhidi yake.
Miongoni mwa bidhaa hizo za Marekani ambazo zimeongezewa ushuru mkubwa wa forodha ni bidhaa za chuma, matunda ya tufaha na lozi (almonds) pamoja na jozi (walnuts).
Mchumi mmoja ameliambia gazeti la Times of India kuwa, kwa kuongezwa ushuru huo kwa bidhaa hizo za Marekani, serikali ya New Delhi itaweza kupokea ushuru wa ziada wa dola milioni 217.
Vita hivi vya kibiashara kati ya New Delhi na Washington viliibuka Machi mwaka jana, baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuongeza kwa asilimia 25 ushuru wa forodha wa bidhaa za chuma zinazoagizwa na Marekani kutoka India, na asilimia 10 kwa bidhaa za alumini. Ushuru huo mpya wa asilimia 25 na 10 kwa bidhaa hizo unazigusa pia nchi za Umoja wa Ulaya, Canada na Mexico, ambazo ni waitifaki wa Washington.
Haya yanajiri siku chache baada ya mazungumzo ya kutatua mvutano wa kibiashara kati ya Marekani na China kuvunjika.
Hii ni katika hali ambayo, hivi karibuni Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alitahadharisha kuhusu kushtadi mivutano ya kibiashara duniani na taathira zake hasi hususan kwa nchi zinazoendelea.
Aidha Mfuko wa Fedha Duniani IMF unaamini kuwa, vita hivyo vya kibiashara vinavyoendelea hivi sasa vimepunguza na kuvuruga uchumi wa dunia na kuibua hali ya kutoamianiana miongoni mwa nchi mbalimbali duniani.