Wamarekani waandamana katika miji 130 wakitaka Rais Donald Trump asailiwe
Wananchi wa Marekani wamefanya maandamano katika miji tofauti inayokaribia 130 wakitaka Rais Donald Trump wa nchi hiyo asailiwe.
Maandamano hayo yaliyoratibiwa na makundi tofauti yanayompinga Trump, yamefanyika ikiwa ni katika kupinga siasa mbovu za rais huyo. Kwa mujibu wa taarifa, maandamano hayo yamefanyika kwa lengo la kukosoa hatua mbovu za Trump ambapo waandamanaji wametaka rais huyo asailiwe mara moja. Mbali na maandamano, makundi hayo ya upinzani yameanzisha tovuti iliyopewa jina la 'Msailini Trump' ambapo ndani yake wamekosoa kitendo cha rais huyo kutumia vibaya madaraka yake ambapo wameeleza kuwa jamii ya Marekani inalitaka bunge la kongresi litekeleze wadhifa wake na kumtia hatiani rais huyo. Wakati huo huo tovuti ya The Mercury News imeripoti kuwa kusini mwa jimbo la California nchini Marekani kumefanyika zaidi ya makongamano 140 dhidi ya Trump na kwamba karibu shakhsia 100 miongoni mwa wapinzani wa mji wa Northampton jimboni Massachusetts wametaka kusailiwa rais huyo.
Aidha mitandao mingine ya habari nchini Marekani imeripoti kujiri maandamano katika majimbo ya Oregon, Washington, Massachusetts na Colorado ambapo washiriki walipeperusha angani puto la utoto wa Trump. Maandamano ya wananchi nchini Marekani yanajiri katika hali ambayo kutolewa ripoti ya Robert Mueller, mpelelezi maalumu wa faili la uingiliaji wa Russia katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2016 nchini humo, kumezidisha mashinikizo ya kuanzishwa mwenendo wa kusailiwa rais huyo wa Marekani.