UN haijaafiki madai ya Marekani kuhusu drone yake iliyoangushwa na Iran
Umoja wa Mataifa umejibu madai ya wakuu wa Marekani kuwa drone yao ya kijasusi iliyoangushwa na Iran iliangushwa katika maji ya kimataifa katika Ghuba ya Uajemi.
Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema hana mamlaka wala uwezo wa kubaini ilikoanguka drone hiyo ya Marekani.
Guterres pia ameashiria hatua ya kutunguliwa drone ya kijasusi ya Marekani katika anga ya Iran na kubainisha wasiwasi wake kuhusu kuenea taharuki katika eneo la Ghuba ya Uajemi.
Jana Iran ilionyesha mabaki ya ndege isiyo na rubani (drone) ya kijasusi ya Marekani ambayo ilitunguliwa mapema Alhamisi baada ya kukiuka anga ya Iran.
Kamanda wa Kitengo cha Angani cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu Brigedia Jenerali Amir Ali Hajizadeh alihutubia waandishi habari wakati wa kuonyesha mabaki ya drone hiyo. Amesema drone hiyo ya kijasusi ya Marekani ilionywa mara kadhaa baada ya kukiuka anga ya Iran na kwamba onyo la mwisho lilitolewa 9:55 Alhamisi alfajiri, dakika 10 kabla ya kutunguliwa.
Aidha alitoa maelezo kamili kuhusu harakati za drone hiyo ambayo ilianza shughuli zake za ujasusi saa sita na dakika 14 mapema Alhamisi ikitokea katika uwanja mmoja wa ndege za kivita katika Umoja wa Falme za Kiarabu kabla ya kutunguliwa 10:05 karibu na Kouh-e-Mobarak katika eneo la Jask mkoani Hormozgan kusini mwa Iran.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo Iran imezitoa za mfumo wa kimataifa wa GPS, drone hiyo ya kijasusi ya Marekani ilikuwa katika anga ya Iran wakati wa kutunguliwa. Marekani haijaweza kutoa ushahidi wowote wa maana kuthibitisha madai yake kuwa eti drone hiyo ilitunguliwa katika anga ya kimataifa.