Russia yalaani vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran
Vikwazo vya upande mmoja dhidi ya Iran ni vikwazo vilivyo kinyume cha sheria na vinavyokinzana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. Nchi za kundi la 4+1 limelaani vikwazo hivyo dhidi ya Iran.
Kuhusiana na suala hilo, Rais Vladimir Putin wa Russia juzi Alhamisi Juni 20 alisisitiza kuwa vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya Iran havina msingi wowote. Putin amebainisha kuwa: Iran imeheshimu na kufungamana na ahadi na majukumu yake pia kuhusiana na makubaliano hayo hata baada ya Marekani kujitoa katika makubaliano hayo ya nyuklia; na ndio maana nchi za kundi la 4+1 zinatambua kuwa vikwazo hivyo vya Marekani dhidi ya Iran havina msingi wowote. Wakati huo huo Putin ametahadharisha kuhusu kuongezeka mivutano kati ya Marekani na Iran katika eneo la Ghuba ya Uajemi na taathira mbaya za mivutano hiyo katika eneo.
Marekani iliiwekea Iran vikwazo katika marhala mbili yaani Agosti na Novemba mwaka jana baada ya Trump kutangaza kujitoa kwa upande mmoja kwenye makubaliano hayo ya nyuklia Mei Nane mwaka jana. Ni wazi kuwa vikwazo hivyo ni vya upande mmoja na vyenye kukiuka sheria za kimataifa likiwemo azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Baada ya kutekelezwa vikwazo hivyo vya upande mmoja; Washington iliiwekea pia Iran vikwazo mbalimbali vya kiuchumi, kifedha, kibiashara na nishati hata hivyo haijaweza kuifanya Iran isalimu amri mbele ya matakwa yake.
Iran imekuwa ikisititiza mara kwa mara kwamba kamwe haitalazimishwa na Marekani kuketi nayo kwenye meza ya mazungumzo na si nchi ambayo inaweza kusalimu amri mbele ya matakwa ya dola la kibeberu. Marekani imepuuza waziwazi hata misingi ya haki za binadamu katika kutekeleza vikwazo vyake hivyo dhidi ya Iran; na pamoja na kuwa Iran mara kadhaa imesisitiza kutojumuishwa vikwazo vya dawa na chakula katika vikwazo hivyo lakini makampuni kadhaa yanayozalisha dawa ya Iran pia yamekumbwa na vikwazo katika vile vilivyotangazwa mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu. Jambo hilo linaonyesha kuwa lengo la serikali ya Trump la kutekeleza vikwazo hivyo vya ziada ni kwa ajili ya kuiweka chini ya mashinikizo Iran ili isalimu amri mbele ya matakwa ya Washington ya kupenda kujitanua. Uwekaji vikwazo mbalimbali dhidi ya nchi nyingine khususan mahasimu na wapinzani wa Washington umekuwa wenzo mkuu unaotumiwa katika siasa za nje za Marekani katika kipindi hiki cha utawala wa Rais Donald Trump. Alexander Novak Waziri wa Nishati wa Russia anasema: Dunia nzima imechoka na vikwazo vinavyowekwa na Marekani bila ya udhibiti wowote dhidi ya nchi mbalimbali ambazo viongozi wake hawaridhiwi na Washington.
Kuendelea vikwazo hivyo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya nchi mbalimbali kumekabiliwa na upinzani na malalamiko kimataifa. Marekani si tu kuwa inatumia fimbo hiyo ya kuweka vikwazo ili kuzing'oa madarakani serikali halali katika nchi mbalimbali bali inafanya hivyo lengo likiwa ni kutoa pigo kwa mahasimu wake wa kibiashara ili kuhodhi masoko ya uchumi duniani. Moja ya dagadaga zinazozikabili sasa nchi zilizoathiriwa na vikwazo vya serikali ya Trump ni kukabiliana na vikwazo hivyo vya Marekani na kuwasilisha mbinu za kisasa na ubunifu katika uwanja huo sambamba na kuwepo ulazima wa kuanzisha kampeni ili kuzima taathira hasi za vikwazo hivyo vya Washingtom.
Kuhusiana na suala hilo, Nicolai Patrushev Katibu wa Baraza la Usalama la Russia amearifu kuhusu kuungwa mkono pendekezo la Iran la kuasisiwa mfumo wa kimataifa wa kudumu kwa ajili ya kukabiliana na vikwazo vya kidhalimu vya kiuchumi. Patrushev ameeleza hayo pambizoni mwa kikao cha kimataifa cha viongozi wa ngazi za juu wa kiusalama huko Ufa mji mkuu wa Jamhuri ya Bashkortostan.
Patrushev amesema kuwa: Katika kikao hicho Ali Shamkhani Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran ametoa pendekezo zuri katika mashauriano ya kuasisiwa mfumo wa kimataifa wa kukabiliana na vikwazo vya kiuchumi na akasema pendekezo hilo limeungwa mkono na washiriki wote wa kikao cha Ufa.
Kwa msingi huo, inatarajiwa kuwa katika siku chache zijazo nchi zilizowekewa vikwazo na Marekani zitafikia mapatano na kuasisi njia na mifumo mbadala ya pamoja kwa ajili ya kukabiliana na vikwazo hivyo vya Marekani.