Shutuma za Amnesty International kwa siasa za wahajiri za Trump
https://parstoday.ir/sw/news/world-i54430-shutuma_za_amnesty_international_kwa_siasa_za_wahajiri_za_trump
Rais wa Marekani, Donald Trump daima alikuwa akisema katika kampeni za uchaguzi uliopita wa rais kwamba ataweka sheria kali za kuwazuia wageni kuingia Marekani. Hivi sasa maafa ya siasa hizo za kibeberu za Trump yanaonekana uwazi kabisa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 28, 2019 23:32 UTC
  • Shutuma za Amnesty International kwa siasa za wahajiri za Trump

Rais wa Marekani, Donald Trump daima alikuwa akisema katika kampeni za uchaguzi uliopita wa rais kwamba ataweka sheria kali za kuwazuia wageni kuingia Marekani. Hivi sasa maafa ya siasa hizo za kibeberu za Trump yanaonekana uwazi kabisa.

Mwili wa baba mmoja na kitoto chake cha kike cha miezi 23 uliopatikana baada ya kufa maji katika mto unaozitenganisha Marekani na Mexico, kwa mara nyingine umewashtua walimwengu kuhusu hali mbaya ya kibinadamu inayotawala katika mipaka ya Marekani. Baada ya kuenea picha za baba huyo na kibinti chake kichanga, Shirika la Haki za Binadamu la Amnesty International limemshutumu na kumlaumu vikali Donald Trump kwa siasa zake zisizo na chembe ya utu.

Amnesty International limeandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba, kuenea picha za kuogofya za miili ya kitoto kichanga na baba yake katika mpaka wa Marekani kumezidi kutia hofu kuhusu siasa za wahajiri za Donald Trump. Tukio kama hilo huwa linatokea pale viongozi wa nchi wanapofuata siasa za aibu zinazowalazimisha watoto wadogo kuishi katika mashaka na mateso bila ya kutaka. 

Mama na mwanawe raia wa Honduras katika mpaka wa Mexico

 

Kadhia ya wahajiri wanaoingia Marekani kupitia mpaka wa Mexico ni miongoni mwa daghadagha na kilio kikubwa ndani ya Marekani. Inakadiriwa kwamba hivi sasa karibu wahajiri milioni 11 wanaishi nchini Marekani kinyume cha sheria. Katika kampeni zake za uchaguzi, Trump aliahidi kuchukua hatua kali za kukabiliana na wimbi la wahajiri wanaotumia mipaka ya kusini mwa Marekani kuingia nchini humo kimagendo. Miongoni mwa ahadi zilizotolewa na Trump ni kujenga ukuta katika mpaka wa Marekani na Mexico na vile vile kuwafukuza wahajiri wanaoishi Marekani kinyume cha sheria.

Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa,  misimamo hiyo ya Trump ndiyo iliyowavutia wanachama wa chama cha Republican hasa wa majimbo ya kusini mwa nchi hiyo kama vile "Arizona" na "New Mexico" ambao kilio chao kikuu ni suala hilo la wahajiri haramu. 

Mpaka wa Marekani na Mexico

 

Hata hivyo Trump amekuwa akishutumiwa na kulaumiwa vikali kutokana na siasa zake hizo hasa mpango wake wa kutaka kujenga ukuta katika mpaka wa Marekani na Mexico. Licha ya kuweko lawama nyingi dhidi yake, lakini katika miezi ya hivi karibuni, Trump alipendekeza mipango mipya kuhusu siasa za wahajiri. Alkhamisi ya tarehe 16 Mei, rais huyo wa Marekani alisisitizia msimamo wake wa kuchukua hatua kali dhidi ya wahajiri na kujigamba akidai kuwa: "Mapendekezo ya sasa hivi ndiyo kamili zaidi na yaliyokusanya mambo mengi zaidi kuhusu wahajiri kuwahi kutolewa hadi hivi sasa." 

Katika upande mwingine, Trump ameingia kwenye mzozo mkubwa na Mexico na sambamba na kumtishia jirani huyo wa kusini mwa Marekani kwamba atamuwekea vikwazo na kupandisha ushuru wa bidhaa za Mexico zinazoingia Marekani, amemlazimisha rais wa nchi hiyo kuweka maelfu ya wanajeshi mpakani ili kuzuia wahajiri wasiingie Marekani. Hata hivyo Trump amefeli katika siasa zake hizo kama alivyofeli katika siasa zake nyingine zote. Wimbi la wahajiri wanaoingia Marekani kinyume cha sheria bado ni kubwa. Wahajiri hao wanahatarisha maisha yao na ya familia zao kuingia nchini Marekani ili kukimbia hali ngumu ya maisha katika maeneo yao. 

Wahajiri wanahatarisha usalama wa familia zao kukimbilia na kutumia njia hatari kuingia Marekani

 

Baada ya kuenea picha za baba na bintiye waliokufa maji katika mpaka wa majini wa Marekani, Donald Trump amedai kuwa amesikitishwa na vifo hivyo, hata hivyo lakini, hakukiri kwamba yeye ndiye mkosa, bali amekibebesha lawama zote chama cha Democrat ambacho amedai kimekataa kumuunga mkono katika siasa zake za kuzuia wageni kuingia Marekani. 

Bunge la Congress la Marekani liko mikononi mwa chama cha Democrats, na katika kujibu tuhuma za Marekani, spika wa bunge hilo, Nancy Pelosi amesema kuwa siasa za Trump za kutaka kuwafukuza wageni nchini Marekani zimezusha hofu katika nyoyo za watoto wadogo na kwamba siasa hizo ni kinyume na haki za binadamu.  Hata hivyo Trump na licha ya kuonekana wazi balaa la siasa zake dhidi ya wageni, bado anaendelea kung'ang'ania msimamo wake wa kuwafukuza huko Marekani. Pelosi wamesema, siasa hizo za Trump ni za kikatili na hata ikitokezea kufikia mwafaka baina ya vyama viwili vya Democrats na Republican lakini hana imani na Trump na anaamini kuwa hatotekeleza ahadi zake.