Trump abadili msimamo wake kuhusiana na Afghanistan
Rais wa Marekani amebadili msimamo wake kuhusu matamshi aliyotoa katika mahojiano aliyofanyiwa huko nyuma kuhusu kuondoa wanajeshi wa nchi hiyo huko Afghanistan.
Licha ya kudai katika mahojiano na kanali ya habari ya Fox News kwamba ana hamu ya kuondoa wanajeshi wa Marekani waliopo Afghanistan Trump amesema kuwa kuondoka askari wa Marekani nchini humo kutaibadili nchi hiyo kuwa sehemu ya kuimarishwa harakati za magaidi. Rais wa Marekani ameitaja Afghanistan kuwa ni Chuo Kikuu cha Havard cha magaidi na kueleza kuwa tatizo la kuwaondoa wanajeshi wa Marekani huko Afghanistan ni hili kuwa nchi hiyo itageuzwa na kuwa maabara ya magaidi.
Trump aidha amehalalisha msimamo wake huo na kuongeza kuwa majenarali wa Marekani wamemuomba atekeleze mashambulizi dhidi ya Afghanistan badala ya wao kulazimika kupigana nao katika ardhi ya Marekani. Trump alishasema mara kadhaa huko nyuma kuwa anataka kuondoa wanajeshi wa Marekani waliopo Afghanistan. Wakati huo huo watu 36 waliuawa juzi na zaidi ya 90 kujeruhiwa katika shambulio lililofanywa na Taliban katika jengo la Wizara ya Ulinzi ya Afghanistan sambamba na kufanyika duru ya 7 ya mazungumzo ya amani kati ya wawakilishi wa Marekani na kundi la Taliban huko Doha Qatar. Kundi la Taliban limetangaza kuwa litaendelea kutekeleza mashambulizi kote nchini Afghanistan madhali wanajeshi wa nchi ajinabi khususan wa Marekani wapo nchini humo.