Russia: Marekani haina haki ya kuikosoa Iran kuhusiana na JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/world-i54692-russia_marekani_haina_haki_ya_kuikosoa_iran_kuhusiana_na_jcpoa
Mwakilishi wa Russia katika Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia IAEA amesema kuwa Marekani haina haki yoyote ya kisheria ya kuikosoa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokana na hatua yake ya kupunguza ahadi zake kuhusiana na mapatano ya kimataifa ya nyuklia mashuhuri kama JCPOA.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 11, 2019 03:48 UTC
  • Russia: Marekani haina haki ya kuikosoa Iran kuhusiana na JCPOA

Mwakilishi wa Russia katika Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia IAEA amesema kuwa Marekani haina haki yoyote ya kisheria ya kuikosoa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokana na hatua yake ya kupunguza ahadi zake kuhusiana na mapatano ya kimataifa ya nyuklia mashuhuri kama JCPOA.

Akifafanua suala hilo, Mikhail Ulyanov alisema jana asubuhi kwamba Marekani ambayo imejitoa kabisa katika mapatano hayo ikidai kwamba yana kasoro nyingi na kwamba ni mabaya zaidi kuwahi kutiwa saini katika historia ya Marekani, haifai na wala haina haki ya kutaka kuilazimisha Iran itekeleze kikamilifu ahadi zake za mapatano hayo.

Mwakilishi huyo wa Russia katika wakala wa IAEA ameendelea kusema kuwa Marekani ambayo imekwepa na kukataa kuteleleza majukumu yake katika mapatano hayo kwa visingizio visivyo na msingi, haina haki ya kuwalazimisha wanachama wengine wa mapatano hayo watekeleze ahadi zao.

Mikhail Ulyanov, mwakilishi wa Russia katika wakala wa IAEA

Kazem Gharibabadi, mwakilishi wa Iran katika wakala wa kimataifa wa IAEA ulio na makao makuu yake huko Vienna mji mkuu wa Austria, amesema kuwa siasa za nje na mienendo ya Marekani ni ya kindumakuwili na kwamba kufanyika kikao cha Magavana wa wakala huo kwa ombi la Marekani ambayo yenyewe imekiuka mapatano ya JCPOA, ni kichekesho kichungu.

Kikao cha dharura cha magavana wa IAEA kilifanyika jana alasiri katika makao makuu ya wakala huo huko Vienna kwa ombi la Marekani, kwa ajili ya kuchunguza hatua za hivi karibuni za Iran kupunguza ahadi zake katika mapatano ya JCPOA, hatua ambazo zimechukuliwa kutokana na hatua ya pande nyingine za mapatano hayo ya kutotekeleza ahadi zao kwa Iran.