Uturuki: Uamuzi wa Marekani unakinzana na moyo wa umoja na ushirikiano
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki ametoa radiamali kuhusiana na uamuzi wa Marekani wa kuiondoa serikali ya Ankara kwenye mpango wa kununua ndege za kivita za F 35 na kusema kuwa, uamuzi huo wa Washington unakinzana na moyo wa umoja na ushirikiano baina yao.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki imebainisha kuwa uamuzi wa viongozi wa Marekani umekosa uhalali wa kisheria. Hii ni katika hali ambayo jana Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilitangaza kuwa, Washington imeiondoa Uturuki kwenye mpango wa mauziano ya ndege hizo za kivita. Kabla ya hapo pia Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki alinukuliwa akisema kuwa, hatua ya Marekani ya kutoikabidhi nchi yake ndege za kivira za F 35, ni wizi wa wazi.
Awali Washington ilitishia kwamba iwapo serikali ya Ankara itanunua mfumo wa makombora wa S 400 kutoka Russia, basi itaiondoa Uturuki kwenye mpango wa mauziano ya ndege hizo za kivita. Wiki iliyopita, Uturuki ilianza kupokea shehena ya kwanza ya mfumo wa makombora wa S 400 kutoka Russia.
Kwa mujibu wa habari hiyo, sehemu ya kwanza ya ngao hiyo ya makombora iliwekwa katika moja ya kambi za jeshi la anga kaskazini magharibi mwa mji mkuu wa Uturuki, Ankara.
Mbali na Marekani kuiondoa Uturuki kwenye mpango wa mauziano hayo ya silaha, imewapa marubani wa Uturuki muhula wa hadi tarehe 31 ya mwezi huu wa Julai, wawe wameondoka nchini Marekani na kurudi nchini kwao.