Mgombea uchaguzi wa Marekani: Trump ni mbaguzi wa rangi
Mgombea mmoja wa uchaguzi wa rais wa Marekani amekosoa vikali utendaji wa Rais Donald Trump wa nchi hiyo na kumtaja kuwa mbaguzi mkubwa wa rangi.
Kwa mujibu wa jarida la Marekani la Deadline, Pete Buttigieg, mgombea aliye na umri wa miaka 37 wa chama cha Democrat wa uchaguzi wa mwaka 2020 wa Marekani alisema jana Jumapili kwamba kizazi chake kimeshuhudia rais wa kwanza mweusi na baada yake rais mwingine mbaguzi wa rangi wakichaguliwa kuingia White House.
Pete Buttigieg amesema kwamba Marekani imeingia katika mkondo mbaya wa kuimarishwa hisia za ubaguzi wa rangi na kwamba ana nia ya kuzungumza na watu weusi na weupe wa nchi hiyo kwa ajili ya kukabiliana na tatizo hilo. Msimamo huo wa Buttigieg unahusiana na Mpango wa Douglas ambao unatokana na fikra ya Frederick Douglass, mwandishi wa magazeti, mwanadiploamsia na aliyekuwa mmoja wa viongozi mashuhuri wa Marekani waliopigana dhidi ya utumwa nchini humo.
Mpango huo unahamasisha uwekezaji katika sekta ya afya na tiba katika matabaka ya watu masikini, kuongezwa bajeti ya mipango ya kuimarisha masomo na mafunzo ya kiraia katika shule za Marekani. Kwa kuwasilisha mpango huo, Buttigieg anatumai kupata uungaji mkono wa watu weusi na wenye asili ya Afrika katika uchaguzi ujao wa Marekani.
Buttigieg ambaye alipigana katika vita vya Afghanistan anapinga vita vya kichokozi na visivyo na mwisho vya Marekani katika pembe tofauti za dunia na kuahidi kwamba iwapo atashinda uchaguzi ujao wa Marekani atairejesha nchi hiyo katika mapatano ya kimataifa ya nyuklia, mashuhuri kama JCPOA.