Wafaransa wataka uchunguzi ufanyike kadhia ya kujiuwa bilionea wa Kimarekani
Mawaziri kadhaa wa Ufaransa wametaka kuanza uchunguzi nchini humo kuhusu bilionea wa Kimarekani ambaye ametajwa kuwa alikuwa akijihusisha na magendo ya kuwauza wasichana na mabinti kwa ajili ya biashara ya ngono; bilionea ambaye alikuwa akimfadhili kifedha Rais Donald Trump wa Marekani.
Marlene Schiappa Waziri wa Jinsia na Adrien Taquet Waziri Mshauri katika Masuala ya Ustawi wa Watoto leo wametoa taarifa ya pamoja wakitaka kuanza uchunguzi kuhusu kuhusika Jeffrey Epstein na magendo ya kuwauza wasichana na mabinti. Mawaziri hao wa Ufaransa wamesisitiza pia kuwa uchunguzi uliofanywa na Marekani umefichua uhusiano wa kifedha wenye kufdhehesha wa Paris na kwa msingi huo wamesema kuna udharura mkubwa kuanza uchunguzi haraka iwezekanavyo nchini UFaransa ili kuweka wazi mambo yote yaliyo nyuma ya pazia.
Hata hivyo Nicole Belloubet Waziri wa Sheria wa Ufaransa amesema kuwa serikali hailazimiki kuchukua uamuzi kuhusu masuala hayo.
Kuhusiana na kadhia hii, kundi moja la mawakili wanaowatetea wahanga watoto walioathirika na utumwa wa ngono kwa jina la " Innocence En Danger" pia limewataka waendesha mashtaka wa Ufaransa kuchunguza suala hilo.
Jeffrey Epstein mfadhili wa fedha wa Rais wa Marekani ambaye alikuwa amefungwa jela kwa tuhuma za kuhusika na magendo ya wasichana na mabinti aliaga dunia Jumamosi iliyopita kwa wakati wa Marekani kwa kile kilichotajwa kuwa ni kujiuwa. Epstein aliyekuwa na umri wa miaka 66 alikuwa na ukaribu na watu wenye ushawishi na wanasiasa.