Maafisa 79 wa Jeshi la Anga la Marekani wamejiua
Ripoti mpya imebaini kuwa, maafisa 79 wa Jeshi la Anga la Marekani wamejiua tokea Januari hadi Julai 2019.
Kwa mujibu wa Televisheni ya Fox News, idadi hiyo kubwa ya maafisa wa Jeshi la Anga la Marekani waliojiua katika kipindi hicho cha miezi sita yamkini ikawa ni imevunja rekodi katika historia ya jeshi hilo. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, kwa wastani wanajeshi 100 wa Marekani wamekuwa wakijiua kila mwaka.
Ripoti hiyo imebaini kuwa Kituo cha Jeshi la Anga cha Shaw huko South Carolina nchini Marekani kitafungwa kwa muda kutokana na maafisa watatu kujiua katika kipindi cha mwaka moja.
Weledi wa mambo wanasema matatizo ya kiakili na hali kadhalika matatizo ya kiuchumi ni kati ya mambo ambayo yanawakumba wanajeshi na mavetarani wa Jeshi la Marekani.
Aidha wanajeshi wengi wa Marekani ambao wamehusika katika mauaji ya raia katika maeneo mengi duniani hukumbwa na matatizo mengi ya kiakili wanaporejea nyumbani pindi inapowabainikia kuwa wamemwaga damu ya watu wasio na hatia wakiwemo wanawake na watoto.