Rex Tillerson akiri ujasusi wa Israel dhidi ya Marekani
Katika matamshi ya ufichuaji siri, aliyoyatoa katika Chuo Kikuu cha Harvard, Rex W. Tillerson, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Marekani ameutuhumu utawala haramu wa Kizayuni kuwa umeipotosha serikali ya Marekani, ikiwa ni katika juhudi za kufikia malengo yake.
Tillerson amesema kuwa, ni kweli Israel ina uhusiano wa karibu na Marekani, lakini katika kuamiliana na Netanyahu, ni lazima kuchukuliwe tahadhari, kwa kuwa Israel ikiamua kufikia lengo fulani na kupata ushirikiano wa Washington katika lengo hilo, hutumia kila mbinu ikiwemo ya kuipa Marekani habari zisizokuwa sahihi. Matamshi ya Rex Tillerson yametolewa katika hali ambayo tangu alipoingia madarakani, Rais Donald Trump amekuwa akiiunga mkono Israel bila ya masharti yoyote. Kujiondoa kwenye mapatano ya nyuklia ya JCPOA, mpango wa Muamala wa Karne, kuutangaza mji wa Quds kuwa ni mji mkuu wa utawala haramu wa Kizayuni na juhudi zake za kuzishawishi nchi nyingine zihamishie balozi zao katika mji wa Quds, ni miongoni mwa masuala ambayo yalitekelezwa na Trump kwa matakwa ya utawala khabithi wa Israel. Kuhusiana na suala la mapatano ya nyuklia ya JCPOA, Trump pia alishirikiana kwa karibu na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel, ambapo aliyataja mapatano hayo kuwa ni mapatano mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya Marekani na hatimaye kupitia matakwa ya utawala wa Kizayuni, akaamua kuiondoa nchi yake katika mapatano hayo ya kimataifa hapo mwezi Mei mwaka jana na kisha kuiwekea vikwazo vikali ambavyo havijawahi kushuhudiwa Jamhuri ya Kiislamu.
Kuhusiana na kadhia ya Muamala wa Karne pia viongozi wa ngazi za juu wa utawala haramu wa Kizayuni hususan Benjamin Netanyahu waliongoza kampeni ya kumchochea Trump atekeleze hatua ambayo haikuwahi kutekelezwa na marais wote wa hapo kabla wa Marekani. Hata hivyo licha ya juhudi kubwa zinazofanywa na Trump kwa ajili ya kuufanikisha mpango huo ambao unadhamini moja kwa moja maslahi ya utawala wa Kizayuni, lakini mpango huo umeshindwa kabisa kufikia malengo yaliyokusudiwa. Katika uwanja huo Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anasema: "Hakuna dhamana yoyote kwamba tunaweza kufungua fundo la mjadala wa Israel na Palestina. Ninaweza kusema kuwa, takriban mpango huu (Muamala wa Karne) hauwezi kutekelezwa." Kadhalika mwezi Disemba mwaka 2017 Trump alichukua uamuzi usio wa kisheria wa kuutangaza mji wa Quds kuwa mji mkuu mpya wa utawala haramu wa Kizayuni. Uamuzi huo hata kama ulitekelezwa mwezi Mei mwaka jana na serikali ya Washington, lakini nchi nyingine za dunia si tu kwamba hazikuunga mkono, bali zilitangaza upinzani wao dhidi yake. Licha ya juhudi zote hizo za kila upande za serikali ya Trump kwa maslahi ya Israel, lakini utawala huo wa Kizayuni umekuwa ukiihadaa Washington na kuipatia taarifa potofu na za uongo serikali hiyo ambayo ni mshirika wake mkuu. Katika uwanja huo, jarida la Politiko limefichua habari ya ujasusi unaofanywa na utawala wa Israel kwa amri ya Benjamin Netanyahu dhidi ya watumishi wa ikulu ya Marekani (White House) sambamba na kudukua maongezi ya simu ya watu wa karibu na Trump. Jarida hilo liliandika taarifa hiyo tarehe 12 ya mwezi huu kwa kuwanukuu viongozi watatu wastaafu nchini Marekani ambao wamefichua kuwa ili kudukua maongezi ya rais huyo wa Marekani na viongozi wengine wa ngazi za juu wa nchi hiyo, utawala haramu wa Kizayuni uliweka vifaa vya ujasusi katika maeneo muhimu ya Washington ikiwemo karibu na White House.
Hata kama utawala wa Kizayuni umekadhibisha taarifa ya jarida la Politiko, lakini suala la utawala wa Israel kuwafanyia ujasusi hata mshirika wake wa karibu (yaani Marekani) ni suala ambalo limekuwepo kwa muda mrefu. Mara ya mwisho kugunduliwa ujasusi wa Israel dhidi ya Marekani inarejea kwenye tukio la Jonathan Pollard, Yahudi ambaye alikuwa akifanya kazi katika kitengo cha intelijensia cha jeshi la wanamaji la Marekani ambapo katika nusu ya kwanza ya muongo wa 1980 aliamuriwa na utawala wa Kizayuni kuipeleleza Marekani. Baada ya kugunduliwa ujasusi wake Jonathan Pollard, alihukumiwa kifungo cha maisha nchini Marekani ambapo mwaka 1998 utawala wa Kizayuni ulikiri rasmi kuwa Yahudi huyo alikuwa akifanya ujasusi kwa maslahi ya Tel Aviv. Jasusi huyo aliachiliwa huru katika uongozi wa Barack Obama, rais wa zamani wa Marekani. Kiujumla ni kwamba utawala haramu wa Kizayuni unajifanya kuwa unatekeleza hatua hizo kwa maslahi ya muitifaki wake huyo (Marekani), lakini ukweli ni kwamba Tel Aviv inafanya hayo kwa maslahi yake binafsi. Katika uwanja huo Israel inafanya jitihada kubwa kuwapotosha viongozi wa White House, ingawa viongozi wenyewe wa Marekani wanapinga suala hilo. Kuhusiana na suala hilo Rex Tillerson anasema: "Kwangu mimi ni jambo la kuchukiza kuona mmoja wa waitifaki wetu (Israel) ambaye ni mshirika wetu wa karibu na muhimu, anatufanyia vitendo kama hivi."