Binti wa Kiislamu alazimishwa kuvua hijabu kabla ya kuabiri ndege Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i56244-binti_wa_kiislamu_alazimishwa_kuvua_hijabu_kabla_ya_kuabiri_ndege_marekani
Binti wa Kiislamu ambaye anachezea timu ya taifa ya mchezo wa squash ya Marekani amewafungulia mashitaka wafanyakazi wa shirika la ndege la Air Canada kwa kumlazimisha kuvua hijabu kabla ya kuabiri ndege ya shirika hilo nchini Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 26, 2019 00:43 UTC
  • Binti wa Kiislamu alazimishwa kuvua hijabu kabla ya kuabiri ndege Marekani

Binti wa Kiislamu ambaye anachezea timu ya taifa ya mchezo wa squash ya Marekani amewafungulia mashitaka wafanyakazi wa shirika la ndege la Air Canada kwa kumlazimisha kuvua hijabu kabla ya kuabiri ndege ya shirika hilo nchini Marekani.

Kwa mujibu wa gazeti la The  Independent, Fatima Abdelrahman, mnamo Agosti Mosi alilazimishwa na wafanyakazi hao wa Air Canada kuvua vazi hilo la stara katika Uwanja wa Ndege wa San Fransico jimboni California nchini Marekani, wakidai kuwa hakuwa na hijabu kwenye picha yake ya paspoti.

Binti huyo akiwa na umri wa miaka 12 wakati huo alikuwa anaenda kuliwakilisha taifa lake katika mashindano ya kimataifa ya mchezo wa squash mjini Toronto nchini Canada.

Msichana huyo wa Kiislamu ambaye hivi sasa ana miaka 13 ameiambia kanali ya KTVU kuwa, "Nilipigwa na butwaa kulazimishwa kuvua vazi langu la kidini, kuvuliwa hijabu ni sawa na kukatwa kiungo cha mwili wako. Iliniuma sana! Nilihisi nimebanduliwa kutoka kwenye timu yangu, kwa kuwa wenzangu wote walipita bila vizingiti. Hijabu ni sehemu yangu."

Mbunge Mwislamu katika Baraza la Congress la Marekani, Ilhan Omar

Baraza la Uhusiano wa Kiislamu nchini Marekani (CAIR) limeonya kuwa vitendo vya uhalifu vinavyotokana na chuki dhidi ya Waislamu vimeongezeka nchini humo.

Hivi karibuni pia, askari Mwislamu wa kike katika jeshi la Marekani kwa jina Cesilia Valdovinos aliwafungulia mashtaka makamanda wake kwa kumlazimisha kuvua hijabu.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, Mbunge Mwislamu katika Baraza la Congress la Marekani, Ilhan Omar alitetea vazi la staha la mwanamke wa Kiislamu na kusema kuwa, kuvaa vazi hilo kwake ni aina fulani ya muqawama na mapambano.