Uganda yapongeza "Ubunifu wa Amani ya Hormuz" wa Iran
Waziri Mkuu wa Uganda amepongeza na kukaribisha mpango wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa "Ubunifu wa Amani ya Hormuz."
Ruhakana Rugunda amesema hayo katika mazungumzo yake na Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran jana Alkhamisi, pambizoni mwa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, mjini New York na kuongeza kuwa nchi yake ina hamu ya kuboresha uhusiano na Iran.
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliwasilisha mpango mpya wa amani katika eneo la Ghuba ya Uajemi ambao unajulikana kama 'Ubunifu wa Amani wa Hormuz' kwa kifupi HOPE katika hotuba yake kwenye mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, mjini New York.
Nchi kadhaa tayari zimetangaza kuunga mkono mpango huo wa amani wenye lengo la kuimarisha ushirikiano wa kieneo kwa ajili ya kulinda amani na uthabiti katika Ghuba ya Uajemi.
Mbali na kusisitizia umuhimu wa kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa pande mbili kati ya Tehran na Kampala, Waziri Mkuu wa Uganda, Ruhakana Rugunda amemualika Rais Rouhani kushiriki Kongamano la Kusini-Kusini litakalofanyika hivi karibuni katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki. Hali kadhalika amempa Rais Rouhani salamu na ujumbe kutoka kwa mwenzake wa Uganda, Yoweri Museveni.
Kwa upande wake, Dakta Rouhani amesema uhusiano wa nchi mbili hizi ni mzuri, lakini kuna uwanja na fursa ya kuupanua zaidi katika sekta mbalimbali.
Amesisitizia umuhimu wa kuanzishwa uhusiano wa kibenki kati ya Kampala na Tehran, na kubainisha kuwa uhusiano huo utakuwa na nafasi nzuri ya kuboresha ushirikiano wa kibiashara wa pande mbili.