Marekani haijawafungulia mashitaka makasisi 1,700 wa Katoliki waliolawiti watoto
Uchunguzi wa shirika la habari la Associated Press umefichua kuwa, makasisi, maaskofu, mapadri na maafisa wengine 1,700 wa Kanisa Katoliki nchini Marekani wanaishi huru bila kufuatiliwa na vyombo vya sheria, licha ya kukabiliwa na tuhuma za kuwadhalilisha kingono watoto wadogo.
Uchunguzi huo mpya umebaini kuwa, baadhi ya makasisi hao wa Katoliki wanaendelea kufanya kazi katika mashule licha ya kukabiliwa na madai ya kulawiti watoto wadogo wakiwemo wanafunzi katika taasisi hizo za elimu nchini humo.
Hivi karibuni, Dayosisi 130 za Kanisa Katoliki nchini Marekani zilikiri na kuwataja hadharani makasisi na maafisa wengine wa kanisa hilo wanaotuhumiwa kuwafanyia watoto wadogo dhulma za kijinsia tokeo Agosti mwaka jana 2018. Hata hivyo hatua kubwa iliyochukuliwa dhidi yao ni kushushwa hadhi au kuhamishiwa sehemu nyingine za kazi.
Mwishoni mwa mwaka jana, Mwanasheria Mkuu wa jimbo la Illinois nchini Marekani aliwatuhumu makasisi 700 wa Kanisa Katoliki katika jimbo hilo kwamba wamewalawiti watoto, ikiwa ni idadi kubwa mno ikilinganishwa na ile iliyokuwa imetolewa na kanisa hilo huko nyuma. Jimbo la Illinois lilianzisha uchunguzi huo baada ya ripoti ya uchunguzi katika jimbo jingine la Marekani la Pennsylvania kufichua kuwa, makasisi 300 wa kanisa hilo jimboni hapo waliwanajisi au kuwalawiti watoto zaidi ya elfu moja ndani ya miaka 70.
Kuna mamia ya kesi za ubakaji na ulawiti zinazowakabili makasisi wa kanisa hilo, ambazo zimerundikana katika mahakama za Ulaya na Marekani zikisubiri kufanyiwa uchunguzi, jambo ambalo limeshusha hadhi ya Kanisa Katoliki duniani.
Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis anatafakari kuhusu uwezekano wa kuwaruhusu makasisi, maaskofu, mapadri na watawa wa kanisa hilo waoe na kuolewa kwa wale wanaotaka, kinyume kabisa na kanuni ya kihafidhina ya kanisa hilo.