Mkutano wa chuki dhidi ya Uislamu kufanyika katika hoteli ya Trump
https://parstoday.ir/sw/news/world-i56451-mkutano_wa_chuki_dhidi_ya_uislamu_kufanyika_katika_hoteli_ya_trump
Kundi moja lenye chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu nchini Marekani limepanga kufanya hafla katika mkahawa mashuhuri wa Mar-a-Lago unaomilikiwa na Rais Donald Trump.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 06, 2019 04:46 UTC
  • Mkutano wa chuki dhidi ya Uislamu kufanyika katika hoteli ya Trump

Kundi moja lenye chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu nchini Marekani limepanga kufanya hafla katika mkahawa mashuhuri wa Mar-a-Lago unaomilikiwa na Rais Donald Trump.

Muasisi wa kundi hilo la ACT for America, Brigitte Gabriel amesema kiingilio cha hafla hiyo ya kuuponda Uislamu itakayofanyika mwezi ujao wa Novemba ni dola 1,500.

Mwanaharakati huyo mwenye chuki dhidi ya Uislamu amesema alianzisha kundi hilo kama jibu la Shambulizi la Septemba 11, na anafahamika kwa kuongoza maandamano makubwa ya "Matembezi dhidi ya Sheria za Kiislamu" nchini Marekani mwaka 2017.

Ibrahim Hooper, Mkuu wa Mawasiliano wa Baraza la Uhusiano wa Kiislamu nchini Marekani (CAIR) amesema kikundi hicho ni sehemu ya mtandao wa biashara na vuguvugu la chuki dhidi ya Uislamu ya Trump.

Waislamu Marekani wakiandamana kulaani chuki dhidi yao

Hivi karibuni, Baraza la Uhusiano wa Kiislamu nchini Marekani (CAIR) lilionya kuwa vitendo vya uhalifu vinavyotokana na chuki dhidi ya Waislamu vimeongezeka nchini humo kwa kiwango cha kutisha.

Chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu na mashambulio dhidi ya Waislamu na wahajiri yameongezeka mno nchini Marekani tangu baada ya kuingia madarakani Trump mwaka 2017.